
Dar es Salaam. Wewe ni miongoni mwa wale wanaochoma dawa ya mbu na muda huo huo kupanda kitandani kulala yenyewe ikiendelea kutoa moshi?
Kama ndivyo, basi unajiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya pumu, kikohozi cha mara kwa mara na changamoto ya aleji kwa watoto.
Inashauriwa unapochoma dawa hiyo, usubiri kwa saa moja na nusu hadi saa mbili moshi na harufu ya dawa viishe, ndipo uingie chumbani.
Msikie Janeth Joseph. Anasema siku zote huchoma dawa hiyo muda anaokwenda kulala akiamini ndio muda rafiki.
“Nimekuwa nikifanya hivi kwa miezi kadhaa, kila nikichoma napata usingizi mzito, huwa naifurahia ile hali nikiamini inanisaidia kulala,” anasema na kuongeza:
“Wiki iliyopita nilichoma, lakini sikulala kama nifanyavyo siku zote, nikiwa nimekaa kwenye kochi chumbani, ghafla nilipata kizunguzungu na kuhisi nashindwa kupumua.”
Amesema alipiga kelele, mumewe aliyekuwa sebuleni alikuja kwa haraka na kumtoa nje na kuanza kumpepea.
“Nilikuwa kama mtu ambaye damu inataka kutoka puani, nilihisi maumivu makali ndani ya pua, mume wangu alinimwagia maji ya baridi baada ya muda nikawa sawa,” amesema.
Amesema hakujua ni kitu gani kimemtokea, hadi alipokwenda hospitali na daktari akihisi ni presha ndipo daktari akamdadisi mazingira ya chumba chake kama kina hewa ya kutosha, akamueleza anavyochoma dawa za mbu na kulala.
“Niliambiwa tatizo ni moshi ule wa dawa, niache, tangu wakati huo nimekuwa makini sana ninapotaka kuchoma dawa ya mbu,” amesema.
Janeth ni miongoni mwa wengi wanaokutana na changamoto ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mbu za kuchoma bila wao kufahamu na kujikuta wakijitengeneza athari za kiafya.
Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige amesisitiza kwamba haifai kuchoma dawa ya mbu na kulala muda huo huo, akishauri angalau kusubiri dakika 90 hadi dakika 120 ili moshi wote utoke chumbani.
Amesema moshi wa dawa hizo una athari kiafya huku kwa watoto unaweza kuwasababisha udumavu na mzio. Na kwa watu wazima unasababisha pumu na vichomi vya mapafu.
Dk Mzige aliyewahi kuwa mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya kabla ya kustaafu mwaka 2005, amesema unapochoma dawa ya mbu, inapaswa ukae saa moja na nusu hadi saa 2 ndipo uingie chumbani kulala.
“Dawa hizi kama utazitumia bila kufuata taratibu zinaweza kukuletea athari kiafya, moshi wake ukiingia kwenye mapafu, utakaa muda mrefu hata kukusababishia pumu na kukupa kikohozi kisichokwisha,” amesema.
Amesema unapoitumia unapaswa kusubiri hadi ile harufu yote ya dawa iishe chumbani ndipo uingie kulala.
“Ni bora ung’atwe na mbu, kuliko kuvuta hewa isiyo safi ya huu moshi,” amesema Dk Mzige ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa Mshangai PolyClinic.
Dakatari huyo bingwa wa magonjwa ya mfumo wa hewa, anasema kwa mtoto akipata pumu katika mazingira kama hayo, inamsababishia mzio hivyo ni ngumu kupona.
“Mzio ataimeza katika mfumo wa hewa, hizi dawa za mbu za kuchoma, kupuliza au kufukiza zina athari pia kwenye ukuaji wa mtoto, anaweza kudumaa kwa kukosa oksijeni iliyo safi na salama,” amesema,
Amesema kuna maelekezo ya namna kutumia hizo dawa, lakini watu wengi huwa hawasomi na wengi wao kutumia bila kufuata maelekezo.
“Kama nilivyosema awali, kama huwezi kuzingatia maelekezo ya matumizi yake, ni bora ukubali mbu akuume upate malaria utatibiwa utapona lakini sio ujiue mwenyewe kwa moshi,” amesema.
Amesema mtu anapaswa kulala kwenye chumba chenye hewa safi na salama, akibainisha kwamba si moshi wa dawa ya mbu pekee, hata wale wanaolala na majiko ya mkaa au wale wanaovuta moshi wa sigara ni hatari kiafya.
“Moshi wa sigara kwa mama mjamzito atamdhuru mtoto aliye tumboni kwa kuzaa mtoto mwenye udumavu au mwenye saratani.
“Ili suala la hewa safi na salama sio kwenye moshi wa dawa mbu tu, hata katika mioshi mingine, pia kulala na jiko la mkaa, ni vema wananchi wakachukua tahadhari kabla ya athari,” amesema.
Amesema mtu anapolala anapaswa kulala katika chumba kinacho ingiza na kutoa hewa.
“Unapokosa oksijeni ya kutosha, ndiyo pale utasikia watu walilala na kupoteza maisha, baadhi ya watu hawaelewi mazingira yapi yanafaa kulala, wengine hadi kufikia kupoteza maisha,” amesema.