
Wiki iliyopita tuliangazia kidogo kuhusiana na thamani ya fedha kwa huduma au bidhaa unayoinunua. Mara nyingi, wauzaji hujikita kwenye njia ambazo huficha ukweli wa bidhaa au huduma zao, kwa kutumia mwonekano wa kuvutia au lugha ya kuvutia wanunuzi.
Nitajaribu kuelezea baadhi ya mbinu, kwani itakusaidia kuokoa kiasi cha fedha ambacho kinapotea bila kujua kwa kununua huduma au bidhaa ambayo si ya thamani halisi.
Mosi. Wauzaji hutumia mbinu ya kuuza bidhaa feki kama halisi. Katika masoko mengi, bidhaa feki hupakiwa kwa namna ya kuvutia ili zionekane kama chapa maarufu na zenye ubora.
Kwa mfano, simu za chapa maarufu au vifaa vya elektroniki vinaweza kuuzwa kama bidhaa halisi ilhali ni bandia. Mnunuzi asiyefahamu tofauti hii hujikuta amenunua bidhaa yenye bei kubwa na ubora wa chini, akiamini amewekeza kwenye chapa bora.
Pili. Matumizi ya matangazo yanayokosa uwazi. Wauzaji hutumia maneno ya kuvutia kama vile “bora zaidi” au “kiwango cha kimataifa” bila kueleza kwa undani viwango hivyo. Kwa mfano, baadhi ya bidhaa zinatangazwa kuwa na ubora wa hali ya juu bila kuwa na vigezo vyovyote vya kuonesha hilo.
Tatu. Wauzaji hutumia uharaka wa mnunuaji na kufanya asiweze kuwa na nafasi ya kuhoji ubora wa bidhaa au huduma anayoipata. Mathalani, mnunuzi anaweza kutopata thamani ya fedha pale ambapo analazimika kununua vitu kwa dharura, au anapokuwa safarini kwenye usafiri wa umma. Pia pale mnunuaji anapotangaza kutoa punguzo la bidhaa ambalo linamfanya mnunuzi kutopata muda wa kutafuta bei mbadala.
Nne. Malipo kabla. Bidhaa na huduma nyingi zenye malipo kabla huwa kunakuwa na changamoto ya kuletewa bidhaa ama huduma ambayo si ya thamani ya fedha uliyoilipia.
Mathalani unaweza kwenda kwenye mgahawa ukaagiza chakula ukaambiwa lipa kwanza, baada ya kulipa ukaletewa chakula kidogo, hakijaiva au sicho ulichoagiza, nk. Na wauzaji watakuambia ndicho ulichoagiza, ndicho kipimo chetu, ngoja nikaulize na hutamwona tena na ulishalipia.
Tano. Wauzaji hutumia mbinu ya kucheza na vipimo na viwango vya bidhaa. Mara nyingi, vipimo vya bidhaa vinabadilishwa kidogo, kwa mfano, chupa ya lita moja inaweza kupunguzwa hadi mililita 900, lakini kuuzwa kwa bei inayofanana na ya lita moja. Hii humwacha mnunuzi akiamini amenunua bidhaa ya kawaida, ilhali amepata kidogo kuliko anavyofikiria. Mbinu hii huwanufaisha wauzaji kwa kuuza bidhaa ndogo kwa bei ya kawaida.
Sita. Kubadilisha wafanyakazi. Hii mbinu inatumika pale ambapo mtu ambaye alikuhudumia mwanzo si yule ambaye atalipwa fedha. Kwa maana hiyo unaagiza bidhaa au huduma na unaletewa huduma nyingine tofauti ama chini ya kiwango.
Ukilalamika unaambiwa tu sisi tumeachiwa maelezo kuwa hiki ndicho ulichoagiza. Hapo huwezi kumwona tena yule ambaye ulimwagiza mwanzo au kama ni mawasiliano yanakuwa hayapatikani. Inatokea kwenye sehemu nyingi za huduma. Ni muhimu kujitahidi kila wakati unapofanya manunuzi, inasaidia kupata thamani ya fedha kwa kila unacholipia kwa sababu ndiyo stahiki yako na pia wewe ndiye unajua ni kwa namna gani fedha uliyonayo ulihangaika kuipata.