
Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni, wagonjwa wa viungo ni wengi na hilo halihitaji utafiti mkubwa. Nenda hospitali yoyote kajionee mwenyewe.
Ni kwa nini kuna wagonjwa wengi? Sababu ni nyingi, lakini mojawapo ni namna watu tunavyoishi maisha yetu ya kila siku.
Umejichuguza namna unavyokaa ukiwa darasani, ofisini au uwanjani? Je, umejichunguza unavyolala na namna ya ubebaji wako wa vitu vizito? Makala haya yatakusaidia kujua mikao unayopaswa kuiepuka.
Wataalamu wanataja walio katika hatari ni pamoja na watu wanaofanya kazi zinazohusisha kukaa kwa muda mrefu, ikiwemo wafanya kazi wa ofisini, bodaboda na madereva wa bajaji na magari, mafundi nguo na wengineo ambao shughuli zao zinahusisha kukaa.
Pia watu wenye uzito mkubwa, wasiofanya mazoezi au kujishughulisha na kazi zozote pamoja na wabebaji wa mizigo mikubwa.
Mtaalamu wa Fiziotherapia kutoka hospitali ya CCBRT iliyopo jijini Dar es Salaam, Dk Andrew Charles anasema kuwa kwa ujumla maumivu ya mgongo yanasababishwa na kubadilika kwa uwiano kati ya misuli ya mgongo na tumbo.
Anasema ili mtu asipate changamoto ya maumivu ya mgongo misuli ya tumbo na mgongo inatakiwa kuwa katika uwiano ulio sahihi, hivyo inapotokea changamoto yoyote katika uwiano huo unaweza kusababisha mtu kupata changamoto ya mgongo.
Anabainisha visababishi vinavyoweza kuvuruga uwiano huo kuwa ni pamoja na ukaaji usio sahihi wa muda mrefu bila kunyanyuka, uzito mkubwa, kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi.
“Pia sababu nyingine zinazoweza kusababisha ugonjwa huo ni pamoja na ajali, tabia ya kunyanyua vitu vizito, ujauzito pamoja na tabia ya mtu kukaa tu bila kujishughulisha.
Anaeleza kuwa mkao usio sahihi wakati mtu akifanya shughuli mbalimbali ikiwemo zile za kiofisi, wakati wa safari au wakati wa kuendesha chombo cha moto unamuweka katika hatari ya kupata maumivu ya mgongo.
Anaeleza hicho ni moja kati ya kisababishi cha maumivu ya mgongo kwa watu wengi, hasa wale ambao shughuli zao zinahusisha kukaa kwa muda mrefu.
“Baadhi ya watu huwa wanakosea wakati wa kukaa, wanakalia mgongo badala ya makalio, kwa kufanya hivyo wanajiweka katika hatari ya kupata changamoto ya mgongo, pia aina ya viti pamoja na meza wanazokalia huweza kupelekea changamoto hiyo.
Pia kukaa kwa muda mrefu bila ya kunyanyuka au kutembea tembea kutoka sehemu moja au nyingine
Vilevile anasema mtu anapokuwa na uzito mkubwa utafanya mgongo na magoti nao kupokea uzito mkubwa pale mtu anapokaa, kusimama au kuchuchumaa au kufanya mambo mengine kwa muda mrefu, jambo ambalo linamuweka katika hatari ya kupata maumivu ya mgongo.
Dk Charles anashauri watu wanaofanya kazi zinazohusisha kukaa kwa muda mrefu wajitahidi kuhakikisha wanakaa katika mkao sahihi na kila baada ya muda wa angalau dakika 45 hadi saa moja wananyanyuka kujinyoosha au kutembea kidogo.
“Ili kujua umekaa katika mkao sahihi ni muhimu kuhakikisha mgongo wako umetengeneza umbo la S, pia kuwa na tabia ya kufanya mazoezi,” anaeleza.
Vilevile anasisitiza watu kuepuka tabia ambazo zinaweza kuwaweka katika hatari ya kupata maumivu hayo ambazo ni pamoja na kubeba mizigo mizito, kufanya kazi kwa kuinama au kuchuchumaa kwa muda mrefu.
Maumivu ya mgongo ni ugonjwa unaotajwa kuwa ni zaidi ya asilimia 75 hadi 80 ya magonjwa yote duniani.
Daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo, mishipa ya fahamu wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Laurent Lemery anasema maumivu ya mgongo, kuna wakati mgonjwa anaweza kuyapata katika miguu, kiuno kutokana na pingili kupinda.
Anasema pingili hukandamiza neva za fahamu, lakini anaweza kupata maumivu ya uti wa mgongo baina ya pingili kwa kuwa kuna sehemu ambayo ni laini.
Kwa mujibu wa Dk Lemery, wanapokea watu wenye tatizo la maumivu ya mgongo wenye umri kuanzia miaka 35 na kuendelea.
“Tunaowapokea ni wagonjwa 25 kwa siku wenye miaka 35 na kuendelea na malalamiko yanafanana, atakwambia anaumwa mgongo na wengine ukiwafanyia vipimo unagundua diski zimetoka anatakiwa kufanyiwa upasuaji na wengine misuli imekaza,” anasema.
Wagonjwa hao wameelezwa kuwa hupata maumivu ya mgongo yanayoanzia kiunoni hadi kwenye nyonga pamoja na ganzi kwenye miguu.
Dk Lemery anasema kinachosababisha watu kupata changamoto hiyo ni mfumo wa maisha, alikitolea mfano vijana wanaosoma wakiwa wamekaa kuanzia asubuhi hadi jioni, huku wengine wakitumia muda wao kuperuzi simu na luninga bila kufanya mazoezi.
Pia anasema aina ya ukaaji pamoja na viti vinachangia tatizo hilo, alitolea mfano kuna viti vya chini sana vinasababisha mgandamizo wa diski.
“Tunapaswa kutumia viti ambavyo ni salama kwa migongo yetu, ili kuepukana na tatizo hilo,” anasema.
Anasema kitaalamu dakika za kukaa zinategemeana na uzito, umri na afya ya mtu na kwamba makadirio ni kati ya dakika 45 hadi saa nne.
Mkuu wa Idara ya Fiziotherapia hospitali ya Aga Khan, Simion Gundah anasema;
“Fiziotherapia ni ufunguo wa kuishi bila maumivu ya viungo, ambapo uimara wa migongo yetu unasaidia nguvu za maisha yetu. LBP ni tatizo kubwa la afya duniani, linaweza kumuathiri mtu yeyote na mara nyingi haliwezi kubainishwa kwa sababu moja inayojulikana,” anasema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk Isaya Mhando anaeleza kuwa karibu nusu ya wanawake waliowahi kuwa wajawazito hupata tatizo la maumivu ya chini ya kiuno wakati wa ujauzito, hii ni kutokana na mabadiliko ya ujauzito yanayosababisha kuwa na mkao usio wa kawaida na mgandamizo wa misuli na nyuzi zinazoshika mifupa ya kiuno na mgongo.
“Maumivu ya mgongo na kiuno yanaweza kutokea wakati wa ujauzito kwa sababu ya kulainika kwa mishipa unganishi (ligaments). Mabadiliko ya mkao wa ujauzito husababisha kupindika kwa eneo la chini la uti wa mgongo (lordosis) wakati wa kukua kwa tumbo la uzazi.
Waliopitia changamoto hizo wanasema kukaa kwa muda mrefu ilikuwa chanzo. Mwajuma Shabani (68) ambaye alikuwa muajiriwa kwa takribani miaka 15 katika kampuni moja iliyopo jijini Dar es Salaam alipofika umri wa miaka 55 alianza kupata changamoto ya maumivu ya mgongo.
Mwingine ni Sulle John (45), mkazi wa Kimara ambaye anasimulia kuwa kutokana na maumivu ya mgongo aliyokuwa akiyapata ilimlazimu kuacha kufanya kazi kwa muda wa miezi kadhaa.