Arusha. Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa itaadhimishwa Arusha Machi 8, hema lililofungwa katika eneo la mnara wa saa maarufu ‘clock tower’ limekuwa kivutio kwa wananchi je, unafahamu gharama ya kulala kwa usiku mmoja?
Hema hilo lenye kitanda kikubwa, bafu, varanda mbili na uwezo wa kutopitisha maji wakati wa mvua limejengwa kwa siku tatu na kukamilika jana Jumanne Machi 4, 2025.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Machi 5, 2025 Barnabas Richard kutoka kampuni ya Itika Camps ambao ni wamiliki wa hema hilo amesema bei ya kulala hutofautiana kulingana na msimu wa utalii.
“Sisi kampuni yetu kwa sasa inafanya huduma za malazi na kuzungusha watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo kwa wageni tunawatoza Dola za Marekani 315 (Sh822,150) katika kipindi cha msimu wa utalii (high season) na Dola za Marekani 217 (Sh566,370) kipindi mwitikio mdogo (low season) hii ni kwa mtu mmoja na kwa usiku mmoja,”amesema Richard.

Akizungumzia ujenzi wa hema hilo ambalo limekuwa kivutio jijini hapa, Enock Kaniki ambaye ni miongoni mwa wajenzi wake kutoka kampuni ya House of Canvas amesema upekee wa tenti hilo ndiyo umevutia wananchi.
“Sisi tunatengeneza mahema mbalimbali, hili tumechukua siku tatu kulikamilisha na ukiliangalia ni kubwa na halina joto kutokana na uwepo wa nafasi za upepo kupita.
“Juu tumeweka PVC na vitu vingine ambavyo havipitishi maji hata mvua ikinyesha kwa siku nyingi, tunafanya kazi zetu katika hifadhi za Taifa zikiwamo Serengeti, Ngorongoro, Tarangire na Saadan,”amesema.
Richard amesema sababu ya hema hilo la kitalii kufungwa katika eneo la ‘clock tower’ ni mkusanyiko wa watu wengi huku wakilenga kutangaza utalii huo kwa ambao hawajawahi kulala hifadhini.
“Tuliamua kufanya hivi ili kuwaonyesha uhalisia Watanzania wengi ambao hawajawahi kwenda hifadhini, tukiwaambia watalala kwenye hema walione linakuwaje, hii itasaidia kuongeza mwitikio wa Watanzania kujihusisha katika masuala ya utalii,”amesema Richard.

Ameongeza kuwa: “Mwitikio wa wananchi tangu tufunge hema hapa ni mkubwa sana, wengi wanapiga picha na wanachukua video, na tumepata simu za biashara na email (barua pepe) za watu kuulizia hiki kitu.”
Fursa kuongezeka kwa watalii
Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Uhamiaji nchini kuhusu mwenendo wa watalii wanaowasili nchini kwa miaka minne mfululizo idadi yao imeongezeka.
“Mwaka 2021 jumla ya watalii 922,692 waliwasili nchini, mwaka 2022 waliongezeka hadi kufikia 1,454,920 pia mwaka 2023 waliongezeka tena hadi watalii 1,806,359.
“Idadi hiyo iliongezeka tena mwaka 2024 hadi kufikia watalii 2,141,895, ambapo kutoka mwaka 2021 hadi 2024, idadi ya watalii imeongezeka kwa jumla ya 1,219,203,”zimeeleza takwimu hizo za uhamiaji zilizochapishwa katika tovuti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).
Kwa upande wake Kaniki akielezea fursa wanazozipata kutokana na ongezeko la watalii nchini, amesema: “Kwa sasa wageni wameongezeka nchini, wanavyoongezeka, kule hifadhini wanahitaji hema nzuri kama hizi hivyo, na sisi kazi zinaongezeka.”

“Kwa siku tatu tunatengeneza wastani wa mahema hadi 12, kutokana na uhitaji wa eneo husika,”ameongeza Kaniki.
Magdalena Lucas ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa za kitalii katika eneo la clock tower amesema ujenzi wa hema hilo unaongeza watu katika eneo hilo na upande wao biashara zinafanyika.
“Tangu asubuhi watu ni wengi katika eneo hili (clock tower) na wanasimama hapa, inasaidia kutuongezea wateja maana wanaziona na bidhaa zetu wakiwa wanaangalia hilo tenti,”amesema Magdalena.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema mkoa huo unajikita katika kuutangaza utalii na kubadilisha kuwa fursa kwa wananchi kujipatia kipato.
“Sisi tumejikita katika utalii na wananchi wanabadilisha kila fursa zinazotokana na utalii kujipatia kipato. Mbali ya utalii wa vivutio sasa hivi tunajiimarisha katika utalii wa mikutano (conference tourism),”amesema Makonda.