SWALI ambalo huko mtaani mashabiki wanajiuliza ni kwamba, hiyo mechi ya Kariakoo Dabi ipo au haipo? Hiyo ni baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo namba 184 wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025 kabla ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Baada ya mchezo huo kuahirishwa na Yanga kushikilia msimamo wake kwamba haichezi mechi nyingine dhidi ya Simba bali inataka kupewa pointi tatu, ndipo Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alipoitisha kikao na viongozi wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB), Klabu ya Yanga na Simba ili kutatua mgogoro uliopo.
Kikao hicho maalumu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mchezo huo wa Kariakoo Dabi, kilifanyika Alhamisi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
YANGA YATOKA NA MSIMAMO WAKE
Baada ya kikao cha kwanza kilichohusisha viongozi wa Yanga, ilishuhudiwa vigogo wa timu hiyo wakitoka saa 9:21 alasiri, ambapo wengi waligoma kuwa wazungumzaji sana wakimuachia Injinia Hersi Said kusema lolote.
Mara baada ya Hersi kutoka, amesema wamekuwa na kikao kizuri na wizara hiyo chini ya Waziri Kabudi.
Hersi amesema kikao hicho kilikuwa maalum kwa ajenda ya mchezo namba 184 ambao Yanga ilitarajiwa kucheza dhidi ya Simba.
“Uongozi wa Yanga tukiwa kamili na kamati yake ya utendaji tumeonana na mheshimiwa waziri, naibu waziri, katibu mkuu, naibu katibu mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa.

“Klabu ya Yanga imepata nafasi ya kufikisha yale ya msingi kabisa kutokana na mchezo ule na baada ya kufanya hivyo dhamira ya wizara ilikuwa kutaka kusikia kipi kinatoka kwa uongozi wa Yanga.
“Sisi kama viongozi jukumu letu ni kusimamia maslahi ya taasisi yetu ambayo taasisi yetu inasimamia wanachama na timu kwa ujumla.
“Kwahiyo tulikwenda kufikisha ujumbe wetu kuhusiana na msimamo wetu kama taasisi, Waziri na timu yake ikatusikiliza na wakapata ya kuuliza maswali na tukawajibu.
“Waziri amekuja na mwanzo mzuri akituambia nafasi hii sio kwamba ni eneo la kufanya uamuzi isipokuwa ni nafasi ya kutafuta suluhu juu ya tatizo lililotokea na akitaka kujifunza kutoka kwa Yanga nini hasa kimetusibu.
“Tumeweza kufikisha yote ambayo tulistahili kuyafikisha kama viongozi ambayo yanabeba ujumbe kama Kamati ya Utendaji na ujumbe wa wapenzi na mashabiki wetu nchi nzima.
“Ujumbe huu umemfikia waziri na timu yake wameupokea, tumewaachia waufanyie kazi na tumekubaliana tutakuwa na vikao endelevu ili kupata suluhu ya jambo hili.

“Nichukue fursa hii kuwaaambia wanachama na mashabiki wa Yanga sisi tupo hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya klabu yetu, niwatoe hofu kwa namna yoyote kwamba viongozi wao ni imara na wako hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya taasisi, wakae kwa kutulia, suluhu itakayopatikana tutarudi kwao kuwajulisha,” alisema Hersi.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinabainisha kuwa Yanga wamebaki na msimamo wao uleule wa kutocheza mechi nyingine dhidi ya Simba bali wanataka kupewa pointi tatu.
Hata hivyo, taarifa hizo zimebainisha kwamba Waziri Kabudi amewaambia viongozi wa Yanga kikao hicho si kwa ajili ya kufanya uamuzi bali ni kusikiliza pande zote kabla ya kuangalia uwezekano wa kupata suluhu.
SIMBA WAINGIA SAA 9:23
Dakika mbili baada ya Yanga kutoka kikaoni, saa 9:23 alasiri, Simba nao wakaingia kwa ajili ya kufanya kikao na Waziri Kabudi sambamba na timu yake. Kikao cha Simba na Waziri kilipomalizika, ilikuwa zamu ya viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi.

NJE YA UWANJA
Nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, kulikuwa na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuonana na viongozi wao na kutaka kufahamu nini wameenda kujadili.
Mashabiki hao walitulia pale walipowaona Injinia Hersi na Arafat Haji wakitoka kisha kupata neno kutoka kwa viongozi wao hao.
Hersi alizungumza na mashabiki hao kwa ufupi akiwaambia: “Wananchi eeeeh, si mko sawa? Nyie mlituchagua kuisimamia Yanga. Asanteni.”
Baada ya hapo, gari alilopanda Injinia Hersi na Arafat likaondoka huku mashabiki wa Yanga wakilisukuma na kuimba ‘hatuchezi, hatuchezi, hatuchezi.’