
Neno “Saumu” kwa muktadha wa lugha ya Kiarabu lina maana nyingi, zikiwemo: kujizuia na jambo fulani au kujiepusha na kitu.
Allah amesema kuhusu Mariam: “Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ya kufunga, kwa hivyo leo sitasema na mtu yeyote.” (19: 26) Katika aya hii, neno “Saumu” limetumika kwa maana ya kilugha ya kujizuia kusema.
Saumu kisharia ni kufunga kwa nia ya kujizuia na mambo maalum katika muda maalum kutoka kwa mtu maalum kwa masharti maalum.
Saumu ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu na ibada bora kabisa. Allah Mtukufu ameihusisha ibada ya Saumu na Yeye kama ilivyokuja katika Hadithi Qudsi:”Kila amali ya mwanadamu ni yake, isipokuwa Saumu, hakika hiyo ni Yangu, namimi (mwenyewe) nitalipa malipo yake…” (Bukhar na Muslim). Ni ibada isiyo na muonekano wa nje, bali ni siri kati ya mja na Mola wake. Katika Saumu, kuna dhana ya uchaji Allah wa kweli kwa sababu hakuna nafasi ya ria (kujionyesha).
Maana ya uchajimungu kupitia Saumu
Saumu inamfunza mja kumcha Allah kwa kutii amri zake na kujizuia kwa ajili yake. Hili ni lengo tukufu ambalo Qur’an imetaja mwisho wa aya ya Saumu kwa kusema: “… Ili mpate kuwa wachamungu.”(2:183).
Hii inaonyesha kuwa uchamungu (taqwa) ni hekima kuu ya Saumu na ni lengo la Sharia ya Kiislamu kwa ujumla. Uchajimugu ni kujizuia na matamanio na maovu ya nafsi, ambayo ni msingi wa kila jambo katika Uislamu.
Sayyid Qutb – Allah Amrehemu amesema: “Hivi ndivyo lengo kubwa la Saumu linavyojitokeza – uchaji Allah. Ni uchaji unaochemka ndani ya nyoyo wakati zinapofunga kwa ajili ya kutii amri ya Allah Mtukufu na kutafuta radhi zake.
Uchaji huu ndiyo unaozilinda nyoyo zisiharibu Saumu kwa maasi, hata yale yanayopita akilini. Wale waliokusudiwa na Qur’an wanajua thamani ya uchaji Allah Mtukufu na uzito wake katika mizani yake. Hivyo basi, Saumu inakuwa ni chombo cha kufikia lengo hili tukufu.”
Ikiwa hakuna kingine katika mwezi wa Ramadhani isipokuwa kwamba ni nguzo ya Uislamu, hiyo peke yake ingelitosha kuonyesha utukufu wake. Ni ibada pekee iliyopewa Allah Mtukufu moja kwa moja miongoni mwa amali za wanadamu.
Hekima ya kufaradhishwa Saumu
Mosi, Saumu inabana njia za shetani ndani ya mwili wa mwanadamu, na mara nyingi humzuia na tabia mbaya.
Mbili, Saumu hujenga huruma kwa masikini – mfungaji huhisi hali ya wale wanaoteseka kwa njaa na umasikini katika maisha yao.
Tatu, Saumu humfunza mfungaji kuacha mambo anayoyapenda kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu.
Nne, Saumu humsaidia mfungaji kuyashinda mazoea mabaya na kuwa na uvumilivu mbele ya matatizo.
Tano, Saumu huuimarisha afya na kumkinga mtu dhidi ya maradhi kama unene kupita kiasi, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, na mengine yanayotokana na kula kupita kiasi.
Saumu ina nguzo mbili: moja, nia. Nia lazima iwepo tangu usiku, kwani nia inahitajika katika kila ibada. Mbili, kujizuia na vitu vinavyobatilisha saumu. Mfungaji anapaswa kujiepusha na vyote vinavyobatilisha saumu, kama kula, kunywa, na tendo la ndoa.
Nani hapaswi kufunga?
Kuna wanaoruhusiwa kufungua na lakini wanawajibika kulipa fidia Watu wa kundi hili wanaruhusiwa kufungua, lakini wanawajibika kulipa fidia kwa kulisha masikini kila siku wanayofungua. Hawa ni vikongwe. Ikiwa saumu inawapa taabu kubwa na kuwafanya wapate shida kwa kila msimu wa mwaka.
Wagonjwa wasiotarajiwa kupona – Ikiwa ugonjwa wake hauna matumaini ya kupona, basi anaruhusiwa kufungua na analazimika kutoa fidia.
Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha: Ibn Kathir amesema kuhusu Sharia ya wanawake hawa, wanazuoni wametofautiana kiufahamu:
Baadhi wamesema wafungue, lakini watoe fidia ya kulisha masikini pamoja na kulipa siku walizoacha.
Wengine wamesema walipe fidia tu bila kulipa siku walizoacha. Wengine wamesema: watalipa siku walizoacha bila fidia. Kwa upande wangu ndio mtazamo sahihi. Allah ndiye mjuzi zaidi.
Fidia hapa inamaanisha kumlisha masikini mmoja kibaba kimoja (gramu 544) katika chakula kinachotumika katika mji husika (madhehebu ya Shafi) kwa kila siku iliyofunguliwa.
Pili, wanaoruhusiwa kufungua na kuwajibika kulipa baadaye. Watu wa kundi hili wanaruhusiwa kufungua lakini wanapaswa kulipa Saumu baadaye. Hawa ni wagonjwa wanaotarajiwa kupona,
Wengine ni wasafiri – Msafiri anaruhusiwa kufungua, lakini anapaswa kulipa siku alizoacha.
Safari inayoruhusu kufungua ni ile inayoruhusu kupunguza rakaa za faradhi (qasr). Hili linahusiana na safari inayojulikana katika jamii husika kama “safari” bila kuhitaji kupimwa kwa idadi ya maili au kilomita maalum.