
Dar es Salaam. Nyuki ni mdudu wa ajabu sana. Kwanza ana mbawa ndogo kulinganisha na mwili wake. Inashangaza jinsi anavyoweza kuzitumia mbawa hizo kuubeba na kusafirisha angani mwili wake mzito. Akiwa nchi kavu na angani hukutana na misukosuko ya ndege, mijusi na vyura wanaomwinda kwa ajili ya kitoweo. Kwa bahati nyuki ameumbwa akiwa na rangi kali na silaha ya ncha kali kujihami na adui zake. Wakati mwingine maadui huusikia mvumo wake kama ilani.
Halafu nyuki huishi kwenye jamii inayofikia maelfu kwenye kila jamii. Kila jamii hutambuana kwa kutumia harufu itokanayo na malkia, na kila malkia huwa na harufu yake tofauti. Ikitokea nyuki amepotea na akaingia kwenye jamii ingine, wale vibarua wenyeji watamuangalia kuwa kaja na nini.
Kama amebeba chakula watashukuru “mgeni njoo mwenyeji apone”. Watamuacha aweke chakula, na kama si mkorofi watamwacha aondoke. Kila nyuki anajua wajibu wake. Malkia ni mama anayetaga mayai ambayo baadaye hutotoa watoto. Anakuwa na walinzi kwa masaa yote huku wafanyakazi wengine wakiwajibika kujenga na kukarabati mizinga.
Hao ndio wanaotafuta chakula na malighafi ya zao lao kuu, asali. Lakini pamoja na mzinga wa nyuki kubeba mamia ya vyumba vidogo, nyuki hapotei chumba hata iwe usiku wa manane. Anaweza kurudi na kuingia tunduni kwa kasi ileile aliyotoka nayo angani.
Asali ni zao muhimu sana kwa viumbe wengine wakiwemo binadamu. Mpaka leo hakuna ushahidi maalum wa viungo kamili vinavyounda asali. Tunachoweza kujua ni kuwa nyuki huchukua baadhi ya viungo kwenye maua, kisha huvichanganya na vitu gani sijui hadi asali ikatokea. Lakini asali imethibitika kubeba sukari, maji, asidi, madini na vitu vingine chungu nzima ambavyo vingine hutokana na yeye mwenyewe.
Ajabu ya asali ni dawa inayofanya kazi kwa uhakika. Lile neno “honeymoon” linatokana na utamaduni wa watu waliooana kula asali ili kuongeza uzazi baada ya ndoa. Halafu asali ina dutu inayosaidia ubongo kufanya kazi vizuri, pia ni miongoni mwa vyakula vichache duniani vinavyoweza kukimu maisha ya mwanadamu bila kuchanganywa na kitu kingine. Kumbuka hapa tunazungumzia asali ya asili isiyochanganywa na kitu kingine chochote.
Kijiko kikubwa cha asali kinatosha kumweka mtu hai kwa saa 24. Inasemwa kuwa nyuki waliwaokoa watu kutokana na njaa barani Afrika. Kubwa zaidi, asali haina tarehe ya mwisho wa matumizi. Hata miili ya wafalme wakubwa duniani ilizikwa kwenye majeneza ya dhahabu, kisha kufunikwa na asali ili kuzuia kuoza. Sijui manemane ya Wayahudi ilikuwa ni kitu gani hasa, lakini nikiambiwa ilikuwa asali sitashangaa kabisa.
Kwa kuwa binadamu naye ni kiumbe kama nyuki, anayo mengi sana ya kujifunza kwa mdudu huyu. Kufanya kazi kwa bidii, kuweka akiba, kutunza ekolojia na kujitegemea kwa ubunifu wake ni baadhi tu ya mambo hayo. Nyuki anaishi kwa muda mfupi sana, pengine ni chini ya siku 40. Maishani mwake anatembelea angalau maua 1,000, na hutoa chini ya kijiko kimoja tu cha asali. Lakini kwa kuwa wanafanya kazi kwa nguvu na ushirika, hawajawahi kupungukiwa.
Kitu alichojaliwa mwanadamu ni uwezo wa kuyasoma maisha ya viumbe wengine. Lakini alicholaaniwa ni kutofuata kanuni za maisha ya asili. Binadamu hupenda kuishi kama anavyotamani mwenyewe na si kama anavyopaswa kuishi. Iwapo angeishika kanuni ya nyuki, hakika asingeshindwa na jambo. Tunaona jinsi nyuki aliyekaa kwenye nafasi ya ufanyakazi asivyolazimisha kuhamia kwenye nafasi ya ulinzi.
Kosa kubwa ambalo binadamu anastahili kulijutia ni kuiweka fedha kama kipaumbele chake. Wapo watu wenye karama za tiba asilia. Lakini sababu inayochangia kuharibu afya za watu ni waganga kuingia kwenye tamaa ya kipato zaidi ya huduma yao. Na hata wapatapo kile wanachostahili, watu wengine (wafanyabiashara na madalali) wanajiweka kwenye mbadala wa watoa tiba na kuharibu utaratibu mzima.
Umeona mfano wa “honeymoon” hapo juu. Pamoja na nyuki kuishi kwa muda mfupi, uzao wake hupokea majukumu na kuyatekeleza kikamilifu. Nadhani nguvu yake ya uzazi itokanayo na asali ni ya uhakika. Binadamu wanalijua hilo lakini kwa tamaa ya fedha, wanaongopeana na tiba ya dawa zisizo na kichwa wala miguu. Leo wanalia na upungufu wa nguvu za kiume na ubovu wa afya ya akili. Nyuki hana uzembe huo hata kidogo.
Tunaambiwa kuwa tatizo la afya ya akili ni ugonjwa mkubwa wa binadamu wa sasa. Ugonjwa huu husababisha pia upungufu wa nguvu za kiume, hivyo kuzorotesha uzazi. Lakini kama tulivyoona kuwa asali ina dutu inayosaidia ubongo kufanya kazi vizuri.
Hii ni pamoja ya kujenga afya ya akili na kuondoa msongo. Hivyo bila shaka ikitumika vizuri inaweza kuondoa matatizo mengi na kuboresha hali za wanadamu.
Lakini nilitaka kusisitiza uadilifu wa nyuki kwenye majukumu yake. Malkia anabaki kuwa na majukumu yake, walinzi wana yao na wafanyakazi kadhalika. Nisingependa kuona watu waliokaa vizuri kwenye nafasi zao katika kulitumikia Taifa wakagombane kwenye uchaguzi mkuu. Badala yake wakusanye mawazo yao na kuwasaidia wengine. Tuishi kama nyuki ili tusifeli.