Hekaya za Mlevi: Kupima pombe ya mlevi mwaga pombe yake

Dar es Salaam. Ukitaka kupima nguvu ya mlevi mwaga pombe yake. Hata kama alikuwa amezima, kuna nguvu za umeme zitamshtua kwamba kuna mtu anayefanya balaa kwenye kamzigo kake.

Na hata kama alikuwa ametepeta kiasi gani, ghafla atapata nguvu ya kukabiliana na watu zaidi ya watatu kwa pamoja. Hapo anakuwa si yeye ila ni nguvu za ajabu zinamshukia. Waswahili husema “mzuka umempanda”.

Kwa namna hiyohiyo, ukitaka kujua ukali wa mtoto muumize mama yake. Siku hizi huku uswahilini watu wameshasahau maisha ya familia bora inayobeba baba, mama na watoto. 
Enzi zile wazazi walipendana na watoto wao kiukweli. Hata kama palikuwa na watoto wa kurithi, basi si ajabu wasingelijua hilo mpaka ukubwani. Watoto wote wa damu na wa ukoo walikuwa wamoja.  

Sasa ukitaka kumpandisha wazimu mtoto yeyote, mkwaze mzazi wake. Tena ukitaka kukiona kichaa chake halisi mpigie au mtukanie mama yake. Ni nafuu ukimtukana yeye mwenyewe kuliko kumtukania mama kwani utakuwa umewachanganya wote. 

Nilishawahi kutoa hadithi ya mchezaji wa soka kutoka Kanda ya Ziwa aliyeteuliwa kwenye Timu ya Taifa, akasusia timu na kurudi kwao kwa sababu alitukaniwa mama. 

Kisa kilikuwa ni kocha wao aliyekuwa na masihara mengi. Kocha huyo mtoto wa mjini alizoea kuwarushia matusi wachezaji kama njia ya kuwapandisha mori. Alifanya hivyo kimasihara hivyo wachezaji wake walishamzoea. Siku hiyo akayakanyaga kwa mporipori huyo bila kujua kuwa wenzetu hawana masihara ya kipwanipwani. Ilikuwa almanusura ang’olewe meno ya sebuleni. 

Kiuhalisia, mtoto wa kiume alikuwa rafiki mkubwa wa mama, wakati mtoto wa kike alikuwa karibu zaidi na baba. Wachunguzi wa tabia wanasema hii inatokana na hulka ya mtoto wa kiume kulinda na wa kike hulindwa.

Ushahidi unaonekana kule vijijini. Akina mama wanaposafiri au kwenda umbali mrefu, humtanguliza mtoto wa kiume kama mlinzi wao. Haijalishi udogo wa kidume hicho, lakini akitokea mhuni kuuingilia msafara wao kidume kinachachamaa. Inawezekana ni sababu ya ‘mfumo dume’, lakini kuna ukweli kwamba mtoto wa kiume ndiye mlinzi katika jamii yake.

Lakini hivi sasa kuna tofauti kubwa sana.  Mfumo wa maisha umebadilika mazima kutoka ule wa asili mpaka huu kuwa wa kuiga. Wengi wanadai ni kwa sababu ya kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, ambapo mtu anaweza kuingia kwenye tamaduni za wenzake bila hodi. Hali hii imewafanya wengi wetu waige vitu wasivyovijua ili mradi waonekane wanajua. 

Siri kubwa ya mbumbumbu yeyote ni kutaka kujiweka juu kwa kila jambo. Anapomsikia mwenzake akimwaga stori za ughaibuni, atajifanya kuzijua zaidi. Ataangalia filamu na kuona watu wakipeleka kadi na maua kwenye msiba wa kizungu, basi naye atapeleka maua kwenya msiba wa jirani na kuondoka zake. Hajui kuwa hata wazungu waliishi kama sisi, wakakosea na kujiingiza kwenye maisha magumu sana.

Usemi wa “No Hurry in Africa” ulimaanisha kitu kikubwa zaidi ya unavyoeleweka. Watu wanadhani usemi huo ulionesha ni kwa jinsi gani Waafrika walikuwa wavivu. Lakini kinyume chake Waafrika walikuwa wamejaaliwa kwa kila kitu kiasi cha kutolazimika kuishi kwa mbio nyingi. Hapa kuna mtu asiye na kazi lakini analea familia kubwa, lakini kwa wenzetu thubutu yao.

Kutokana na kuiga tamaduni za Kimagharibi bila kuzielewa, tumejikuta tukizibomoa familia kwa kila mtu kujali chake. Ndoa imekuwa si mapenzi tena bali mkataba, ndio maana kumezuka ‘masingo faza’ na ‘masingo maza’. Hawa wanapooana na kujenga familia, kila mmoja hukumbatia watoto wake. Familia inatengeneza tofauti ya ‘watoto wa baba’ na ‘watoto wa mama’. Mzazi anakosa maamuzi juu ya mtoto wa mwenza wake.

Wakati mwingine unaweza kudhani kuwa watoto na wazazi wana uadui. Mtoto wa mama anadiriki kuondoka nyumbani mara tu baba anapoingia, kadhalika yule wa baba hufanya hivyo mara mama anapoingia. Katika hali hii unaweza kusema wazazi wanafanya makosa ya “kumwaga sumu” kwa watoto, hadi mtoto wa mama akamfananisha baba na Dracula mnyonya damu.

Wenzetu wana utamaduni wa kuwaita wazazi wao kwa majina. Mtoto anayerudi kutoka shuleni humsalimia baba yake, “Hi! Eddie!” badala ya “Shikamoo baba!”. Hata ikiwa “Shikamoo” ni salamu ya kitumwa, basi amsalimie kinyumbani “Twa mbombo?”. Si Wanyakyusa tu, makabila yetu yote hayana shikamoo, bali husalimiana “Habari za kazi” au “Umeshindaje”. 

Athari kuwaita wazazi kwa majina yao zinaonekana wazi. Hivi sasa binti anamchamba baba yake kana kwamba yeye ni hawara wa baba huyo. Anadiriki kuvalia kihasara na kumwonesha babaye vile vinavyostahili kufichwa. Shetani anagonga hodi kwa mzee anayemkaribisha na kuharibu shoo. 

Vilevile sio ajabu kidume kumtia vitasa baba hadharani. Hakioni tofauti ya baba na vijana wenzake anaokunywa nao mtaani. Tena si ajabu yeye akajiona ndiye baba kwa vile anailea familia ya mama yake. Na bado, huku tunakoelekea mtoto atamtuma baba yake dukani akimwambia “kimbia mi nataka kuondoka!”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *