Heche: Tupo tayari kwa hatua ngumu kuelekea uchaguzi mkuu

Tarime/Dar. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema chama hicho kipo tayari kutembea katika hatua ngumu inayotarajiwa kufikiwa baada ya kukamilisha utoaji elimu kuhusu msimamo wa bila mabadiliko hakutakuwa na uchaguzi.

Katika kauli yake hiyo, Heche amesema kwa sasa chama hicho kinalenga kuwafikia viongozi wa dini, balozi za mataifa mbalimbali ili kuzielimisha kuhusu msimamo wa ‘No reform, no election.’

Msisitizo wa Heche unajenga msingi wa msimamo wa chama hicho, uliotangazwa jana Jumatano Februari 12, 2025 na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu aliyesema kwa sasa Chadema inaingia kwenye vuguvugu la mabadiliko.

Vuguvugu hilo kwa mujibu wa Lissu, linalenga kushinikiza mabadiliko ya kisera, kisheria na kikatiba ili kuboresha mifumo ya uchaguzi.

Heche ameyasema hayo leo, Alhamisi Februari 13, 2025 alipohutubia wananchi wa Kijiji cha Kitagasembe wilayani Tarime, wakati wa hafla ya kumpokea tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo ndani ya Chadema.

Ametumia jukwaa hilo kusisitiza msimamo wa chama hicho wa kutokwenda kwenye uchaguzi bila mabadiliko ya sheria zinazoruhusu watu washindane na mshindi atangazwe.

“Chadema tumeonyesha mfano kwenye uchaguzi wetu, na tutawafikia viongozi wa kidini kuwaelewesha msimamo wetu na tutazifikia balozi za nchi za nje, kabla ya kuifikia hatua ya pili na sisi tupo tayari kutembea kwenye hatua hiyo ngumu,” amesema.

Heche amesema kwa kushirikiana na Mwenyekiti wake Tundu Lissu, wataongoza wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanakomesha aina yoyote ya kile alichokiita uhuni unaofanyika katika chaguzi dhidi ya wanasiasa wa upinzani.

Jambo muhimu, ameeleza ni kuungwa mkono na wanachama, wafuasi na wananchi.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, hawako tayari kukubali nchi iwe sehemu ya kuishi kwa hofu, badala yake kuwe na ushindani wa hoja na maisha ya amani.

“Sisi kwa mfano mfumo huu mnaousikia wa kanda, ukiangalia Marekani leo, ina majimbo ndio mfumo wetu wa kanda. Kwa hiyo tutafuta hivyo vyeo vya watu vinaitwa Mkuu wa Mkoa kwa sababu ni watu hawana kazi,” amesema.

Hoja nyingine aliyoiibua, amesema ni kubadilisha mfumo wa elimu itakayotolewa kulingana na mazingira ya eneo husika.

“Kwanini mtu wa Singida anayelima alizeti unamfundisha kulima mihogo. Kwa sababu mihogo pale haikui mfundishe kulima alizeti, kuweka kiwanda cha alizeti, auze mafuta duniani,” amesema.