Tarime. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – Bara, John Heche amesema hatima ya kuondoa matatizo yanayowakabili Watanzania iko mikononi mwao wenyewe.
Hivyo, anasema wanapaswa kuamua kwa pamoja kuunga mkono jitihada za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Heche amesema umefika wakati sasa kwa Watanzania kujua kuwa serikali inapaswa kuwajibika kwao tofauti na ilivyo sasa, wengi wanaamini yanayofanywa na serikali ni msaada kwao.
Amesema hali ilivyo sasa, kura ya mwananchi haina sauti akidai kuwa inaibiwa na mwananchi anapokwa madaraka yake hali inayosababisha kutokuwa na sauti bungeni.
Wakati huo huo, makamu mwenyekiti huyo amesema mwaka huu chama hicho kitahakikisha hakuna uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini kama sheria za uchaguzi hazitabadilishwa.
Amesema uamuzi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanakuwa na mamlaka na madaraka ya kuamua nani awe kiongozi wa nchi kwa kutumia chaguzi za haki na demokrasia.

Waendesha pikipiki wakiongoza msafara wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania bara, John Heche kuingia uwanjani mjini Tarime kwaajili ya mkutano wa hadhara. Picha na Beldina Nyakeke
Msimamo huo wa Heche umetolewa siku moja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Stephen Wasira kusema uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba kama ilivyopangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuwataka wananchi kujiandaa kushiriki uchaguzi huo.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara mjini Bunda na Tarime leo, Heche amesema chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kubaini Watanzania wengi wanaishi katika umasikini uliokithiri licha ya Tanzania kuwa na rasiliamli nyingi na za kutosha ambazo zikitumika vema, zinaweza kubadilisha maisha ya kila Mtanzania.
Amesema ili kufanikisha lengo hilo, Watanzania wanatakiwa kukiunga mkono chama hicho huku akisema yeye na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lisu watakuwa mstari wa mbele kuongoza jitihada hizo bila woga.
“Sisi tutakuwa mbele, hatuogopi kifo tutafanya kazi kuhakikisha serikali inayoingia madarakani iwe ya Chadema au ya CCM inaingia kwa haki na demokrasia, lakini hatuwezi kufanya hivyo kama hamtatuunga mkono,” amesema Heche.
Amesema watazungumza na viongozi wa dini, nchi wahisani hata wana CCM wanaoitakia mema nchi ili kuwaunga mkono.
“Uendawazimu ni kufanya jambo hilo hilo kwa njia hizo hizo na kutegemea matokeo tofauti, mimi na Tundu Lisu hatuko tayari kufanya hivyo tulizaliwa siku moja tutaondoka siku moja tunachohitaji ni kuunganisha wananchi katika ajenda hii,” amesema.
Amesema Tanzania ina rasilimali nyingi za kutosha kuliko nchi nyingi lakini hazijatumika ipasavyo huku akisema kinachosababisha rasilimali hizo zisiwanufaishe ni uongozi uliopo madarakani.

Baadhi ya wakazi wa Tarime wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara,picha na Beldina Nyakeke
Heche amesema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, ibara ya nane, Msingi wa madaraka na uongozi wa nchi unatokana na wananchi wenyewe, jambo ambalo kwa muda mrefu halifanyiki na kusababisha wananchi waendelee kuishi kwenye lindi la umasikini.
“Viongozi wameshindwa kusimamia rasiliamli zilizopo ili zitumike kuboresha maisha yetu, kwa ufupi tunaishi katikati ya utajiri tukiwa masikini, tukifanikiwa kurudisha mamlaka kwa wananchi basi wananchi watakuwa na uwezo wa kumchagua kiongozi wamtakakaye vile vile kumuondoa kiongozi huyo kama atashindwa kutimiza wajibu wake,” amesema.
Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Taifa, Patrick Sosopi amesema kwa miaka 60 Serikali ya CCM imekosa kipaumbele hata kwa sekta moja ili waweze kufanya maendeleo kwa asilimia 100.
Katibu Mwenezi wa Bavicha Taifa mstaafu,Twaha Mwaipaya amesema serikali inapaswa kusema walipo watu ambao wametekwa akiwamo Deusdedith Soka ambaye alitekwa zaidi ya miezi mitano iliyopita.
“Tunafikiria kupeleka nguo za wapendwa wetu waliotekwa huko Ikulu kwasababu serikali imeshindwa kusema wenzetu wako …,” amesema kiongozi huyo.
Amesema familia za watu hao zinaishi kwa huzuni na nguo za wapendwa wao kabatini huku wakiwa hawajui nini kinachoendelea katika maisha yao huku waliko kama wako hai.
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Deogratius Mahilinya amesema umasikini wa Watanzania siyo mpango wa Mungu bali ni mpango wa watu wachache wanaotumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi hivyo watanzania wanatakiwa kuikataa hali hiyo.