Heche alivyopokelewa kijijini kwao, matumaini ya vijana

Tarime. Maelfu ya wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na wakazi wa Tarime na maeneo jirani wamekusanyika nyumbani kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Heche alichaguliwa Januari 21, mwaka huu akiwashinda wenzake, Matharo Gekul aliyepata kura 49 na Ezekia Wenje aliyepata kura 372 huku Heche akishinda kwa kura 577.

Mbali na wananchi, wanachama na wafuasi sherehe hizo za kumpongeza Heche pia zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho ngazi ya taifa, kanda, mkoa na wilaya akiwemo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Taifa, Deogratius Mahilinya.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche

Wengine ni Mwenyekiti mstaafu wa Bavicha Taifa, Patrick Sosopi, Katibu Mwenezi mstaafu Bavicha Taifa, Twaha Mwaipaya, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa, Odero Charles na viongozi wengine.

Pamoja na mambo mengine sherehe hizo zilizofanyika leo Alhamisi Februari 13, 2025 ziliongozwa kwa ibada kutoka kwa Askofu wa kanisa la EAGT Kanda ya Ziwa Joseph Maswi.

Watu waliohudhuria sherehe hizo walikula na kunywa huku ikielezwa kuwa ng’ombe kadhaa walichinjwa kufanikisha shughuli hiyo iliyofanyika nyumbani kwao Heche katika kijiji cha Kitagasembe wilayani Tarime.

Jeshi la polisi lilitoa ulinzi wakati wa sherehe hizo kijijini hapo, gari la polisi ambalo ubavuni liliandikwa OCD Sirari ilionekana likizungukazunguka katika eneo hilo.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime, wamesema kuchaguliwa kwa Heche ni ishara kuwa kila mtu ana uwezo wa kuwa kiongozi kwa nafasi yoyote endapo kutakuwa na demokrasia ya kweli katika uchaguzi husika.

“Nakumbuka kipindi Heche anagombea udiwani katika Kata ya Tarime mjini wapo watu waliombeza kwasababu alikuwa hana chochote hasa ikilinganishwa  na mpinzani wake ambaye alikuwa ni tajiri na mfanyabishara maarufu hapa mjini lakini hakukata  tamaa na akaibuka kuwa mshindi,” amesema Matiko Werungu.

Werungu amesema msimamo na kujiamini ni moja ya sababu ya Heche kufikia hatua hiyo, licha ya changamoto mbalimbali alizozipitia tangu alipoanza harakati za uongozi wa kisiasa.

“Kipindi kile anagombea udiwani akiwa kijana mdogo sana aliambiwa hana hata kitanda lakini mambo kama hayo hayakumkatisha tamaa aliendelea kusimamia kile alichokiamini hadi leo tunamuona amefikia ngazi hii ya kitaifa,” ameongeza;

Jamhuri Marwa, amesema Heche amewapa heshima vijana wa Tarime na kwamba anaamini wapo wengi watakaomtumia kama kielelezo cha kufikia malengo yao.

“Huyu sio kwamba ametokea katika familia tajiri lakini ni kwamba alipoingia kwenye siasa alijua anataka nini na alisimamia hapo hapo bila kuyumba,” amesema Marwa.

Rhobi Webiro amemtaka Heche kuendelea kupeperusha vema bendera ya Tarime kwa kuwa mwadilifu kama alivyo siku zote, huku akisema endapo kutakuwa na uchaguzi huru na haki siku zijazo, upo uwezekano wa Heche kuwa kiongozi mkubwa nchini.

Amesema vijana wa Tarime wana imani na Heche na hawatarajii kusikia akiyumbishwa na kubadili msimamo wake kama ambavyo imeshuhudiwa kwa wanasiasa wengine.