
Acha niwape ‘story’ ya yanayomsibu mwanamke. Ninapogombana na mwanaume, anaponipiga makofi, kunikata na visu, kunipiga na mabapa ya panga hata kunitishia kunichoma na bisibisi, dunia nzima itanishikia kiuno.
Wengi wakiwamo wanawake wenzangu watanyanyua midomo yao juu kama chuchunge bila kujua ninachopitia na mahakimu wasiosomea watatoa hukumu zao kwamba mimi ndio tatizo na kwa yaliyonikuta ni lazima mimi ndiye chanzo. Watadai baba wa watu ni mkimya na hana neno na mtu.
Wapo watakaodiriki kushauri kuwa ilinipasa kukaa kimya na ikibidi hata akinibutua au kunifanyia kitendo chochote kiovu nimwambie asante mume wangu nashukuru sana na naomba unisamehe kwa wewe kunikosea. Yote hayo sababu mimi ni mwanamke.
Nikigombana na mwanaume, asilani abadani siruhusiwi kumrudishia kofi alilonipiga, wala kujitetea wakati napigwa, wala kumjibisha natakiwa nitulie tuli anipige mpaka hamu yake iishe na nimuache ataamua yeye mwenyewe aniue au aniache hai.
Endapo nitafanya kinyume na hapo, waja watasema mimi sina heshima na sijafundwa kwetu. Wakati natendwa nilipaswa kuwa kimya, nilipaswa kuwa na subira nikiamini atabadilika na ninapaswa kumuomba msamaha hata kama sio mimi niliyekosea.
Kwa sababu mimi ni mwanamke, sina ruhusa ya kukasirika wala kuwa na hasira. Kwa hiyo, kiwango cha kutokuwa na hatia kwangu kinalingana sawa sawa na kiwango cha ukimya wangu mbele ya dhulma na ukatili wa mwanaume.
Kwa sababu mimi ni mwanamke hata kama mume wangu anachepuka na kuwa na wanawake wengine wengi, eti wazazi na wakwe zangu pamoja na viongozi wa dini wananiambia nivumilie ili kuokoa ndoa yangu kwa sababu Mungu hapendi kuachana.
Pia wanasisitiza kuchepuka ni asili ya mwanaume hata Suleimani alikuwa na wake 300 na masuria 700 hivyo ili kumfanya atulie na mimi inabidi nirudishe lile tumbo langu ‘flat’ alilolikuta wakati ananichumbia, nivae vizuri na nipendeze ili kumvutia hata kama hanihudumii kwa chochote.
Lazima nimfurahishe mume wangu na kumhudumia ili aweze kunipenda tena na pia nisikose mikesha makanisani kunywa na kupaka maji na mafuta ya upako ili maombi yangu ya kumuombea mume wangu yafike kwa haraka mbele ya uso wa Mungu na nikazane nisiache hata atakapobadilika niendelee nisimpe shetani nafasi.
Wakati nafanya yote hayo huyo ninayemuaombea mwenyewe yupo ametingwa na shughuli zake. Yote hayo sababu mimi ni mwanamke!
Kwa kuwa mimi ni mwanamke, kutokana na majanga yanayonisibu katika kutafuta faraja ikatokea nimeanguka dhambini nikamsaliti mume wangu, nitaitwa kahaba ikibidi hata ukoo mzima na dunia nzima ifahamu.
Viongozi wa dini na watoa hukumu wa duniani watasimama kidete kunihukumu kuwa nimefanya chukizo mbele za Mungu, mimi ni mdhambi na ninastahili moto wa Jehanamu. Yote hayo sababu mimi ni mwanamke!
Sina haki ya kutafuta mahali pengine pa kupata upendo na faraja au msaada wa kihisia ninaokosa nyumbani na mwisho walimwengu husisitiza mimi ni mwanamke mpumbavu na nitaivunja nyumba yangu kwa mikono yangu mwenyewe, kwa kuwa tu sijasimama katika nafasi yangu. Yote hayo sababu mimi ni mwanamke!
Kwa sababu hiyo nitapaswa niondoke katika nyumba yangu tuliyojenga sote wawili huku mali zangu zote zikiwa hapo nakuwa nimebaki sina chochote bali akili zangu tu ambazo ili kulinda ndoa zipo kama zimefungiwa ndani ya boksi kichwani mwangu. Hazijapanuka wala kuongezeka chochote hata kama nilikuwa kinara kwenye matokeo ya kidato cha sita au mwanafunzi bora wakati wa kuhitimu degrii yangu ya kwanza. Yote hayo sababu mimi ni mwanamke!
Pamoja na uanamke wangu, inanipasa kuzaa kwa uchungu na kula kwa jasho. Nabeba mimba miezi tisa, nikijifungua siwezi kulala mpaka mtoto alale ndipo nami nijiegeshe kupata japo lepe moja la usingizi.
Bado nitakesha usiku na mtoto na bado nitaamka mapema kuandaa wengine wanaopaswa kwenda shule. Hapo namshukuru Mungu nina kipato ambacho kinaweza kutafuta msaidizi wa kusaidia kazi za nyumbani na kumlipa.
Vinginevyo ingekula kwangu na bado jioni hata kama nimechoka vipi ni lazima kutoa haki ya ndoa kwa mwanaume ambaye huenda amerudi amelewa, hivyo naishia kutoa huku nakuwa kama nabakwa.
Bado haitoshi hata kama nitanyonyesha mtoto usiku mzima bila kupata usingizi wa kutosha ni lazima baba apate haki yake usiku. Kisha asubuhi na mapema niamke nikapambane na mwajiri ili kujiingizia pato la familia. Bado mimi ni mwanamke tu kama wanawake wengine.
Kwa kuwa mimi ni mwanamke bado mwanaume anajiona ana haki ya kunizuia kuwaona watoto wangu niliowazaa ikitokea tumetengana. Miaka kadhaa baadaye, watoto wangu wanatambulishwa kwenye jamii kuwa ni wanaharamu. Sababu tu mimi mama yao ni mwanamke ambaye sina mume.
Baba wa watoto wangu ndio kwanza ana miaka 30 na anamiliki kampuni kubwa sana. Ni tajiri mkubwa, na watu wamemtambulisha kuwa ni mtu mzuri, mtu mwema, mchapakazi, mwenye umakini, mwenye mwelekeo wa taaluma na aliyefanikiwa katika umri mdogo sana. He is a hero. Sababu tu yeye ni mwanaume.
Mimi nina miaka 28, nimefanikiwa na ninamiliki kampuni yangu, lakini kwa kuwa sina mume naonekana sipo makini na maisha.
“Ni mchapakazi na anapenda sana pesa, na sasa anazo pesa za kutosha ila amekosa mume tu.” Wanasikika waja wakizungumza kila ninapopita.
Napigwa na bumbuwazi na kuwaza na kuwazua ikiwa kufanikiwa kuna uhusiano wowote na jinsi ya mtu.
Kwa sababu mimi ni mwanamke, siruhusiwi kuwa na akili, wala kuwa mcheshi, siwezi kuwa na uwezo wa kifedha wala kufanikiwa kitaaluma au kuheshimiwa bila kuwa na mwanaume kando yangu.
Kisha walimwengu bila kujua undani wa maisha ya mtu, watakaa wakiniita malaya kaachika huyo, ndoa imemshinda pamoja na yote bado hajakamilika, hana mume.
Hawaoni uwezekano kwamba huenda nililazimika kupitia heka heka nilizopita ili kufika nilipo, yote kwa sababu mimi ni mwanamke.
Wanasahau kuwa mwanaume akifiwa na mkewe kwa sababu yoyote akioa baada ya miezi sita jamii nzima itaona kwamba alichokifanya ni sahihi anahitaji mwanamke wa kumpa faraja na wa kumsaidia kulea watoto. Atasifiwa na kupongezwa kwani aache wafu wazike wafu wenzao.
Mwanamke akifiwa na mumewe hata akipata mwenza na akaolewa miaka minne baada ya mumewe kufariki utawasikia walimwengu wakimwambia unaolewa “aaah! Mbona mapema sana?
Watabaki wanaulizana, Mna uhakika huyo anayemuoa hakuwa bwana wake wakati mumewe yupo hai? Au yeye ndio alimuua mumewe. Ni mchawi! Kwa sababu tu ni mwanamke.
Wanaume naomba tukumbushane hapa kuwa, mimi kuwa mwanamke, hainifanyi mimi kuwa mtu mdogo!
Mwanamke ni nani?
Mwanamke akiwa amekaa kimya bila kusema chochote ni dhahiri kuwa kuna mamilioni ya mambo yanapita kwenye kichwa chake. Anapokutazama huwa anashangaa kwanini anakupenda sana licha ya watu wengine kukuchukulia kawaida.
Anaposema nitasimama karibu nawe, atasimama karibu nawe kama mwamba imara. Kamwe usimdhuru au kumchukulia poa.
Kuna mtu fulani alimuuliza mwanamke, wewe ni mfanyakazi au mama wa nyumbani? Yule mwanamke akajibu: Ndio, mimi ni mama wa nyumbani anayefanya kazi wakati wote. Ninafanya kazi saa 24 kwa siku. Mimi ni mama. Mimi ni mke. Mimi ni binti. Mimi ni mkwe. Mimi ni saa ya kengele kuwaamsha wanangu kwenda shuleni. Mimi ni mpishi mzuri sana ninayepika chakula cha familia.
Mimi ni mjakazi ambaye lazima nihakikishe kila kitu kimekaa sawa hapa nyumbani. Mimi ni mwalimu ambaye ni lazima nihakiki kile walichofundishwa watoto shuleni na kufanya nao home work pamoja. Mimi ni mhudumu mzuri sana. Mimi ni msaidizi. Mimi ni muuguzi nisiye na zamu pale ambapo kuna mgonjwa ndani ya nyumba yangu. Mimi ni ofisa usalama, ninayehakikisha usalama wa familia.
Mimi ni mshauri. Mimi ni mfariji. Sina likizo hata kama nitakuwa likizo ya kazi za mwajiri. Sipati hata likizo ya ugonjwa sababu hata nikiwa kitandani ni lazima nihakikishe familia yangu imepata chakula. Sina siku ya kupumzika.
Ninafanya kazi mchana na usiku. Ninapokuwa kwenye simu kwa muda mrefu na malipo yangu ni kuulizwa kwa sentensi. “Ninafanya nini muda wote huo?
Mwanamke ni wa kipekee sana, ana tabia za kipekee sana. Namfananisha mwanamke kama chumvi! Uwepo wa chumvi kwenye chakula haukumbukwi wala hauna thamani kamwe kama watu wamekula na kushiba lakini ikitokea chakula hakina chumvi itafanya chakula kikose ladha na wengine kushindwa kukila kabisa. Hapo ndipo thamani ya chumvi huonekana.