Haya ndio matumaini wafanyakazi kuelekea Mei mosi

Unguja. Wakati tukielekea katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc) limeeleza yanayotegemewa kutoka serikalini ikiwa ni pamoja na kupata majibu ya changamoto zao walizowasilisha mwaka jana.

Katika maadhimisho kama hayo mwaka jana, Shirikisho liliwasilisha changamoto 11, hata hivyo kati ya hizo tano hazijapatiwa ufumbuzi hivyo wanatarajia kupata majibu yake mwaka huu.

                                                                                                      Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Aprili 21, 2025, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Khamis Mwinyi Moh’d amesema matarajio yao wapate ufumbuzi kwenye maadhimisho ya mwaka huu.

Miongoni mwa changamoto hizo ni sheria namba 10 ya ajira ya mwaka 2014 ambapo mwajiri hatakiwi kufanya uamuzi bila ya kuwashirikisha wafanyakazi.

Nyingine ni pensheni za wafanyakazi wa Serikali walioajiriwa mwaka 1988/98 kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) walikuwa hawapati pensheni hadi watakapoingia katika mfuko huo.

“Hoja hii tumeshaipeleka Serikalini na imeshaundwa tume na itawasilisha ripoti yake ili nao wapatiwe haki zao, kwa hiyo tunategemea tupate majibu yake,” amesema Moh’d.

Hoja nyingine amesema ni pensheni ya watu wanaostaafu miaka 55, kwa mujibu wa Sheria namba mbili ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2014, mtu akifika miaka hiyo anaweza kustaafu hivyo watu hao wakienda ZSSF wanatakiwa kukatwa kiinua mgongo, jambo ambalo sio sahihi na wametaka sheria hiyo irekebishwe.

Suala la kuchelewa kufanyiwa kazi kikokotoo cha ZSSF baada ya mwaka 2017 kiinua mgongo kupungua na Serikali imekubali kulifanyia kazi jambo hilo, na tayari kuna utafiti unafanyika ambao utaleta majibu namna ya kurekebisha.

“Mwisho ni suala la mfuko wa bima ya afya ambao wafanyakazi wakienda na vitambulisho vyao majina hayaonekani, wakati mwingine wanaambiwa waongeze fedha na kadi kutotumika, hizi ndio hoja tano ambazo hazijafanyiwa kazi,” amesema Khamis. 

Amesema, licha ya changamoto hizo kutofanyiwa kazi pia zipo sita ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi.

“Suala la kulipwa mishahara kwa wanaostahiki, kulipwa kwa madeni sugu kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) na kiwanda cha uchapaji, kuchelewa kurekebisha mishahara hawa ni watu wanaostaafu bila kurekebisha mishahara yao hilo tayari limeshafanyiwa kazi.”

“Suala la uhuru wa kujiunga pamoja kwa maana ya ushirikishwaji katika ngazi za uamuzi na kutatua matatizo yao, Serikali imeshatoa waraka wa kuwaruhusu wafanyakazi kufanya hivyo,”amesema.

Amesema, watendaji waliopewa dhamana ndio wanatakiwa kushughulikia changamoto hizo ili zipatiwe ufumbuzi.

Hivi karibuni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alisema usimamizi na utatuzi wa changamoto za wafanyakazi kwa taasisi husika unahitajika ili kupunguza malalamiko, ambayo yamekuwa tayari yameshasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.

“Kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikilipa kipaumbele suala la stahiki zote muhimu za wafanyakazi kwa kusimamia, kufanya marekebisho na maboresho ya masilahi ya wafanyakazi wa umma kama sheria za utumishi wa serikalini zinavyoelekeza,” amesema Hemed.

Hemed ameahidi Serikali kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shirikisho hilo na kuwa tayari kukutana nao ili kujadili mambo mbalimbali ikiwemo malalamiko yanayohitaji marekebisho ya sheria katika utekelezaji wake ambayo yamekuwa yakichukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa mahotelini, Ali Salum Ali amesema kumekuwa na pengo kubwa kati ya wafanyakazi wa chini na viongozi wao, katika maeneo mengi ya kazi jambo linalosababisha kutokuwa na uhusiano mzuri kazini.

Pia, amesema kuporomoka kwa maadili na utendaji wa kazi jambo hilo linachangiwa na baadhi ya viongozi kutotoa nafasi ya kuwasikiliza watendaji wa ngazi za chini ambao ni watu muhimu katika taasisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *