Haya ndio maeneo makuu yaliyoimarisha elimu Zanzibar

Haya ndio maeneo makuu yaliyoimarisha elimu Zanzibar

Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imetaja mafanikio kadhaa ya kujivunia kutokana na mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika sekta ya elimu, likiwemo ongezeko kubwa la bajeti.

Bajeti ya sekta hiyo imeongezeka kutoka Sh265.5 bilioni mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh830 bilioni kwa mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 212.6.

Ongezeko la bajeti ya sekta ya elimu pia limechangiwa na kuongezeka kwa bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kutoka Sh11.5 bilioni mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh33.4 bilioni mwaka 2024/2025.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein, akijibu hoja ya Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdallah Ameir, katika kikao cha Baraza leo Mei 21, 2025, alieleza mafanikio ya kujivunia katika sekta ya elimu, yaliyotokana na mchango wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Mwakilishi huyo alitaka kufahamu mambo mahsusi yanayoonesha mafanikio ya mabadiliko yaliyofanyika katika sekta hiyo chini ya uongozi wa Rais Mwinyi.

Amesema kuwa pamoja na ongezeko hilo la bajeti, idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo hiyo pia imeongezeka kutoka 4,289 mwaka 2021/2022 hadi kufikia 7,215 mwaka 2024/2025.

Kingine ni kuimarika kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kujenga madarasa 4,120 yanayojumuisha ujenzi wa shule mpya 35 za ghorofa na shule 53 za madarasa ya chini.

“Jumla ya madarasa 1,227 yamefanyiwa ukarabati na jumla ya dakhalia (mabweni) 14 zimejengwa. Katika muktadha huo, Serikali imenunua jumla ya seti 102,671 za viti na meza pamoja na vitanda 1,160 kwa ajili ya dakhalia na kusambazwa katika shule mbalimbali Unguja na Pemba,” amesema.

Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), pia imepewa uzito unaostahiki kwa kununuliwa na kusambazwa kompyuta za mezani 3,002, komputa mpakato 1,051, vishikwambi 6,193, pamoja na projekta 552.

Sambamba na hayo, jumla ya shule tisa zimeunganishwa na Mkonga wa Taifa, kazi hiyo inaendelea kwa kuziunganisha shule 61, vituo 18 vya ubunifu, vituo 10 vya walimu, kituo cha elimu mbadala Rahaleo na maktaba kuu.

Jambo lingine ni kuanza kwa utekelezaji wa mtaala mpya wa umahiri kwa ngazi ya elimu maandalizi, msingi na sekondari ambapo jumla ya vitabu 3,424,436 vya kufundishia na kujifunzia vimenunuliwa kufanikisha utekelezaji wa mtaala huo.

Amesema ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya Taifa umeimarika mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2024 umefikia asilimia 96.66 darasa la saba, asilimia 84.4 kidato cha pili, asilimia 82 kidato cha nne na asilimia 99.9 kidato cha sita.

“Jumla ya wafanyakazi wapya 5,207 wameajiriwa ikijumuisha walimu 83 wa elimu mjumuisho,” amesema Naibu Waziri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *