
Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) umeipa ruhusa Yanga kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (Cas), kupinga uamuzi wa kuahirishwa kwa mchezo wao dhidi ya Simba, uliokuwa uchezwe Machi 08, 2025.
Yanga inaamini uamuzi huo haukuwatendea haki ikidai kwamba, haukufuata kanuni na ulilenga kuibeba Simba ambayo ilitangaza kutokuwa tayari kucheza kwa sababu tu, ilizuiwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, siku moja kabla kama kanuni zinavyoeleza.
Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto amenukuliwa na Mwananchi Digital akisema kuwa hawaizuii Yanga kwenda Cas, lakini walipaswa kusubiri hadi bodi itoe uamuzi juu ya suala hilo.
“Cas! huwezi kuzungumza tu Cas ni rahisi lakini ina taratibu zake. Lakini, kwa sababu wenzetu walishawahi kwenda Cas kwa suala la Morrison (Bernard) sina shaka wanajua hizo taratibu na watazipitia. Kwa hiyo wanakwenda Cas, huwezi kumkataza mtu ila kikubwa sisi ni kuja kujibu kama tutaitwa. Majibu ya kuwapa Cas tunayo na wakati huo kama tumeshafanya uamuzi wetu, tutapeleka kwamba ilikuwa ni hivi,” amenukuliwa Mnguto.
Hata hivyo, Yanga inaripotiwa kuwa tayari imeshapeleka malalamiko yake Cas yakiambatana na kiasi cha Dola 40,000 (Sh106 milioni) ambayo ni ada ya kuendeshea kesi hiyo.
Wakati Yanga wakisubiri kufahamu tarehe ya kusikilizwa kwa shauri hilo pamoja na jopo la wasuluhishi, muongozo wa uendeshaji mashauri wa Cas unampa mamlaka Mfaransa Carole Malinvaud wa kuamua ni lini na akina nani watamaliza mjadala juu ya suala hilo.
Idadi ya wasuluhishi inaweza kuanzia mmoja hadi watatu na wanachaguliwa na Rais wa kitengo husika, ambaye kwa sasa ni Malinvaud.
“Rais wa Kitengo ataamua nambari hiyo, kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo. Kisha Rais anaweza kuteua msuluhishi pekee wakati mlalamishi anapoomba hivyo na mlalamikiwa hatalipa sehemu yake ya malipo ya awali ya gharama ndani ya muda uliowekwa na Ofisi ya Mahakama ya CAS,” imefafanua ibara ya 40.1 ya muongozo wa Cas.
Malinvaud ni gwiji wa sheria za kimataifa za biashara na pia usuluhishi wa migogoro. Ni mhitimu wa vyuo maarufu vya sheria vya Paris II Ufaransa na Shule ya Sheria ya Havard, Marekani.
Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara ya Ufaransa ambayo amehudumu kuanzia 2013. Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la mchezo wa gofu.
Malinvaud atateua msuluhishi/wasuluhishi kutoka katika kundi la wasuluhishi 171 wa Cas ambao, miongoni mwao kuna raia saba kutoka Bara la Afrika.
Waafrika ambao miongoni mwao wanaweza kuteuliwa kuamua suala la Yanga ni Tshiamo Rantao na Terence Dambe (Botswana), Paul Pretorius, Tembeka Ngcukaitobi na Poobalan Govindasamy (Afrika Kusini), Wellington Magaya (Zimbabwe) pamoja na Abdallah Shehata wa Misri.