Dar es Salaam. Wakati leo Machi 3, 2025 ikiwa ni Siku ya Wanyamapori Duniani (WWD), imebainika kuwa, baadhi wanaongoza kwa kuua watu wengi kwa mwaka, jambo ambalo limetengeneza uhasimu na binadamu.
Siku hii huadhimishwa kila mwaka kutambua mchango wa kila mnyama na mimea katika ustawi wa binadamu. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ufadhili wa Uhifadhi wa Wanyamapori: Wekeza kwa Watu na Dunia.”
Licha ya umuhimu wa kila kiumbe katika ikolojia, binadamu wamekuwa wakikabiliwa na hatari kwa kuuawa na baadhi ya wanyama, matukio ya vifo hivyo yamekuwa yakiripotiwa kwa idadi kubwa kila mwaka.

Kwa mujibu wa BBC Science Focus, mbu ndiyo kiumbe anayeua zaidi binadamu, kwa mwaka anaua takribani watu 725,000.
Mbu anaeneza Ugonjwa wa Malaria ambao ndiyo umekuwa ukiua watu wengi.
Itakumbukwa kuwa mbu jike ndiyo hatari zaidi kwa ugonjwa huo.
Anayeshika nafasi ya pili katika kuua watu wengi ni binadamu wenyewe kupitia matukio ya mauaji yanayotokea kila siku.

Inakadiriwa kwamba watu 400,000 wanauawa na binadamu wenzao kila mwaka duniani kote.
Katika nchi za Amerika ya Kusini, mauaji ni mengi ukilinganisha na maeneo mengine duniani. Mauaji katika nchi ya El Salvador yanafikia asilimia saba ya vifo.
Mnyama anayeshika nafasi ya tatu kwa kuua watu wengi ni nyoka. Mnyama huyu anayepatikana sehemu mbalimbali duniani, anakadiriwa kuua watu 138,000 kwa mwaka.
Nyoka wana sumu kali na wamekuwa wakiwauma binadamu na kusababisha vifo vyao.

Vifo vya kawaida vya binadamu vinavyosababishwa na nyoka hutokea kutokana na kuumwa na sumu, hata hivyo, inaweza kusababisha kukatwa viungo na kupata ulemavu mwingine wa kudumu, kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO).
Mbwa nao wanafuatia katika kundi hili kwa kusababisha vifo vya watu 59,000 kwa mwaka kupitia ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Licha ya kwamba mbwa ni rafiki wa binadamu, wamekuwa wakihatarisha maisha yao.
Wakati vifo vinavyotokana na kushambuliwa na mbwa vikiwa si vya kawaida, vifo vya binadamu kutokana na kichaa cha mbwa vinavyoenezwa na kuumwa na mbwa si jambo la kawaida kusikika, hasa vinatokea katika nchi maskini zaidi duniani ikiwa ni pamoja na Afrika na Asia.
Kwa mujibu wa WHO, mbwa ndio chanzo kikuu cha vifo vinavyotokana na kichaa cha mbwa, na huchangia hadi asilimia 99 ya maambukizi yote ya kichaa cha mbwa kwa binadamu.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa mate kupitia kuumwa, mikwaruzo na kugusana moja kwa moja na maeneo yaliyoathirika kwa mbwa.
Kiumbe mwingine ni nge ambaye anakadiriwa kuua watu 3,300 kwa mwaka.

Nge akikutana na adui yake anamuuma na kuingiza sumu yake inayomdhoofisha adui na kusababisha kifo chake mara moja.
Licha ya kuwepo kwa aina zaidi ya 2,600 za nge, ni aina 25 pekee ndiyo wanaweza kusababisha kifo kwa sababu wana sumu kali inayoweza kumwangamiza binadamu.
Mamba nao hawajabaki nyuma, ripoti ya BBC Science Focus inaeleza kwamba, husababisha vifo 1,000 vya binadamu. Meno yao makali na nguvu nyingi ndiyo vinawapa uwezo wa kuwaua watu katika maeneo ya mito au maziwa wanamoishi.
Tembo wanaua watu 600 kwa mwaka na kuwa kwenye orodha ya wanyamapori wakali wanaoua watu.
Ukubwa wake umekuwa ukiwezesha kuwashambulia watu na kusababisha madhara kwao.
Mnyama mwingine mkali ni kiboko anayekadiriwa kuua watu 500 kwa mwaka.
Viboko hutumia meno yao yenye ncha kali (hadi nusu mita) kupigana na anaweza kuuma mtu mara moja tu katikati na kumtenganisha.
Uumaji wa kiboko una nguvu ya psi 1,800, karibu mara tatu ya simba.
Simba na ukali wake, naye anafuatia katika nafasi za nyuma kwa kuua watu 200 kwa mwaka.
Mnyama huyu amekuwa akichukuliwa kama hatari zaidi kuliko wengine, lakini anaua watu wachache ukilinganisha na wengine waliotangulia.