Hatua zichukuliwe kuporomoka ghorofa Kariakoo

Tukio la kuanguka kwa jengo la ghorofa nne eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ni maafa yaliyowagusa Watanzania na Taifa kwa jumla.

Kufuatia janga hilo lililotokea Novemba 16 mwaka huu, hadi jana watu 20 wamethibitika kupoteza maisha na zaidi ya 80 kujeruhiwa.

Janga hili limetuonyesha upungufu wa kiutendaji katika usimamizi wa ujenzi na uzembe wa baadhi ya watendaji wa Serikali. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na majeruhi awape uponyaji wa haraka waweze kuendelea na shughuli zao.

Tukio hili limefungua mjadala mpana kuhusu masuala ya usalama wa majengo, ujenzi holela na uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa Serikali katika kusimamia mipango miji.

Suala hili limekuwa linaimbwa kila mara yatokeapo maafa yanayofanana na hili, lakini utekelezaji hauonekani. Hilo ndilo linasukuma kuitaka Serikali ichukue hatua za kisheria kwa yeyote ambaye hakutimiza wajibu wake, iwe mmiliki wa jengo, wahandisi au watendaji wa Serikali ambao kwa namna moja au nyingine, wamehusika na uzembe uliopelekea maafa hayo.

Uwajibikaji wa kisheria kwa watakaobainika kuhusika katika tukio hilo, unapaswa kuwa wazi na kuhakikisha hakuna mtu anayekwepa wajibu wake katika suala hili. Hatua kali za kisheria zinapaswa kuchukuliwa ili kuonyesha kuwa usalama wa raia hautaachwa mikononi mwa uzembe wa aina yoyote, uwe wa binafsi au wa kimfumo.

Vilevile, hatua zisiishie hapo, huo uwe ndio mwanzo wa kuchukua hatua kwa wanaokiuka kanuni za ujenzi iwe Kariakoo au mahali pengine.

Tumewasikia wataalamu wa ujenzi, wakieleza kuwa misingi ya majengo mengi ya Kariakoo ilijengwa kwa kiwango cha kubeba ghorofa chache, lakini kutokana na ongezeko la mahitaji, wamiliki wamekuwa wakiongeza ghorofa bila kuzingatia uwezo wa msingi wa jengo na wengine wameongeza vyumba chini ya ardhi ambavyo havikuwa kwenye michoro ya awali.

Mabadiliko haya ya matumizi ya majengo pamoja na kubadilisha ya hoteli au makazi ya watu kuwa ya kuhifadhi mizigo, yamekuwa mambo ya kawaida Kariakoo na hapana shaka kwamba yanaathiri uimara wa jengo na kusababisha maafa makubwa.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan aliyetembelea eneo la tukio na kutoa pole kwa majeruhi, alionesha dhamira ya kutatua tatizo hilo kwa undani.

Tunasimama na kauli yake kuhusu kuchukua hatua, tukiamini itakuwa kweli baada ya tume inayochunguza usalama wa majengo ya Kariakoo kuhitimisha kazi yake na kuwa ripoti haitawekwa kabatini kama ilivyotokea kwa tume zilizotangulia.

Mathalani, hatujasahau ripoti ya tume iliyoundwa mwaka 2013, iliyobainisha kuwa majengo mengi yamejengwa kinyume cha sheria.

Janga hili mbali na kufunua uzembea huo, linatoa funzo kubwa kuhusu umuhimu wa usimamizi wa sheria za ujenzi, hasa katika maeneo yenye msongamano wa watu na tukisimamia hilo, nchi yetu itapiga hatua kubwa mbele.

Kama Rais Samia alivyoeleza, mchakato wa utoaji vibali vya ujenzi unapaswa kuwa wa kina na lazima usimamiwe kwa ukamilifu na asiyefanya hivyo amulikwe bila kuchelewa.

Watendaji na wataalamu wa ujenzi wasimamie kutekeleza sheria kuhakikisha ujenzi wa ghorofa na majengo mengine unafuata taratibu zake na msukumo wa mashindano ya kibiashara au shinikizo la wawekezaji.