Hatimaye Mukwala kaanza

Baada ya Mwanaspoti kuripoti namna mastaa wa zamani wa Simba wanavyotamani kuona kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akimuanzisha Steven Mukwala dhidi ya Al Masry na kumuweka benchi Leonel Ateba, hatimaye yametimia.

Fadlu amewajibu wale wote waliotamani kumuona Mukwala akianza katika mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali unaotarajiwa kuanzia saa 10:00 jioni hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika kikosi cha Simba kinachoanza kwa ajili kuikabili Al Masry, Mukwala ataongoza eneo la ushambuliaji huku Ateba akianzia benchini.

Hiyo ni tofauti na ilivyokuwa mchezo wa kwanza ugenini nchini Misri ambapko Ateba alianza na kucheza kwa dakika 80 kabla ya kumpisha Mukwala wakati Simba ikipoteza kwa mabao 2-0.

Ateba amekuwa chaguo la kwanza kwa Fadlu msimu huu akicheza mechi zote tisa za kimataifa kwa dakika 635 akifunga mabao matatu na asisti moja wakati Mukwala akicheza nne pekee akitumia dakika 141.

Kitendo cha Mukwala kuanza badala ya Ateba, kimefanya kikosi cha Simba leo kuwa na mabadiliko ya mchezaji mmoja pekee kutoka kile kilichocheza na Al Masry Jumatano iliyopita.

Hiki hapa kikosi cha Simba kinachoanza leo; Moussa Camara, Shomari Salum Kapombe, Mohamed Hussein Mohamed, Abdurazak Mohamed Hamza, Karaboue Chamou, Yusuph Ally Kagoma, Elie Mpanzu Nkibisawala, Fabrice Luamba Ngoma, Steven Dese Mukwala, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis Prosper.

Wanaoanzia benchini ni Ally Salim Juma Khatoro, David Frank Kameta, Leonel Ateba Mbida, Debora Mavambo, Awesu Awesu, Joshua Mutale, Valentin Nouma, Ladaki Juma Chasambi na Edwin Charles Balua.

Simba inahitaji ushindi wa angalau mabao 3-0 ili kufuzu moja kwa moja nusu fainali ya michuano hiyo lakini kama ikimaliza kwa ushindi wa 2-0, itapigwa mikwaju ya penalti kumpata mshindi. Ikishindwa kufikia malengo hayo safari yao itaishia hapo ikiwa ni mara ya sita kushindwa kufuzu nusu fainali michuano ya CAF katika misimu saba kuanzia 2018-2019.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *