Hatimaye Bashe, Kijaji, Tax na Pindi Chana wamefikiwa

Dodoma. Bunge la Bajeti linaendelea tena kesho, Machi 19, 2025 jijini Dodoma na mawaziri wanne wanatarajiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa macho na masikio ya wengi huenda yakaangazia zaidi kwenye wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, sambamba na ile ya Maliasili na Utalii.

Mbali ya wizara hizo, nyingine ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Wachambuzi wa mambo wanasema huenda mijadala mikubwa inatarajiwa kuibuka kuhusu maendeleo ya mazao, mbolea ya ruzuku, mbegu za asili, miradi ya umwagiliaji, vifungashio, korosho na huenda sakata la mazao mipakani likaibuliwa tena kwa upande wa Wizara ya Kilimo.

Wakizungumzia Wizara ya Maliasili na Utalii, wanasema suala la mipaka kati ya vijiji na hifadhi bado ni kilio kwa wabunge, uvamizi wa wanyama kwenye makazi ya watu na suala la fidia au kifuta machozi ambacho hutolewa baada ya wanyama kuharibu mazao au kujeruhi watu, kimekuwa kikiibuliwa kila mara na wabunge wanapochangia hoja za wizara hiyo.

Wizara pekee ambayo huenda ikawa na mteremko kama ilivyo miaka yote ni ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Lakini kwa upande wa Wizara ya Mifugo, suala la majosho limeibuka mara nyingi kwenye maswali na hoja za wabunge, uzuiaji wa shughuli za uvuvi katika baadhi ya maziwa, na vyombo vitumiwavyo kwa shughuli za uvuvi.

Wizara inayoanzisha safari ya wiki hii ni Wizara ya Maliasili na Utalii, itakayojadiliwa kwa siku moja.

Tangu kuanza kwa mkutano huu wa Bunge la Bajeti, suala la uvamizi wa tembo limeendelea kuwa gumzo, likirejea kwa nguvu baada ya kuibuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023 na Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete, pamoja na Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka.

Wabunge hao walieleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanyama hao wanaovamia makazi ya watu na mashamba.

Hali ilizidi kuwa tete wiki iliyopita, pale Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita, alipoliambia Bunge kuwa jimbo lake linakabiliwa na uharibifu mkubwa unaofanywa na tembo ambao wanaendelea kuharibu mashamba na kuhatarisha maisha ya wananchi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, hata jana tu katika jimbo langu, tembo wameua mtu. Hali ni mbaya sana, tunaomba sana msaada wenu kuwaondoa wanyama hawa na kuwarudisha kwenye hifadhi walikotoka,” alisisitiza Ole Lekaita.

Sambamba na kilio cha tembo, suala la mipaka ya hifadhi limeibuka tena bungeni.

Wabunge wengi wamekuwa wakilalamikia utekelezaji mdogo wa mapendekezo ya Kamati ya Mawaziri Wanane iliyozunguka nchi nzima kukusanya maoni katika maeneo yenye migogoro ya mipaka.

Kamati hiyo ilipendekeza kuongezwa kwa baadhi ya maeneo ya mipaka ili kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na kadhia hiyo, mkazi anayeishi karibu na hifadhi ya pori la Mkungunero, Abllah Cholo, amesema wamechoka na ahadi za Serikali.

“Hao wabunge na mawaziri wote ni kama wanatuzubaisha. Hivi kama Rais Magufuli (DkJohn) alishasema waje kutuongezea vipande kwa kunyoosha mipaka kipindi kile kabla hajafa, lakini wanakaa kimya, ina maana wanakiuka maagizo na miongozo ya wakubwa wao,” amesema Cholo kwa hasira.

Cholo aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kijiji kwa miaka 15, ameongeza kuwa kilio kuhusu mipaka kimekuwa kikubwa kwa muda mrefu.

Amesema idadi ya watu katika maeneo hayo imeongezeka kwa kasi, wakati idadi ya wanyama imepungua, lakini maeneo ya hifadhi yamebaki kuwa yale yale, hivyo kusababisha msongamano na migogoro.

Kwenye Wizara ya Uvuvi, suala la kifuta machozi kutokana na watu waliouawa na mamba na kufungwa kwa muda kwa maziwa kwenye shughuli za uvuvi pia huenda likajadiliwa.

Kilimo, Korosho

Ukiachilia mbali miradi ya kilimo kama BBT na suala la biashara ya mazao ndani na nje ya nchi, jambo lingine ambalo huenda likaibuka bungeni ni biashara ya zao la korosho, ambalo limekuwa na ufanisi mzuri katika msimu huu huku likiwa na mipango mikubwa ndani ya miaka mitano ijayo.

Msimu wa mwaka 2024/2025, Tanzania iliweka rekodi ya mauzo makubwa ya korosho nje ya nchi kiasi cha Dola za Marekani karibu 583.7 milioni (Sh1.57 trilioni) baada ya uzalishaji wa korosho ghafi kufikia kiasi cha tani 528,260.

Kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na tani 254,500 zilizouzwa katika msimu uliopita na kuingizia nchi kiasi cha Dola 221.3 milioni (Sh598.72 bilioni).

Kiasi kikubwa kuwahi kuzalishwa ni tani 313,000 zilizozalishwa katika msimu wa 2017/2018.

Katika msimu wa 2024/2025, kati ya korosho zote zilizozalishwa, tani 410,000 ziliuzwa nje ya nchi huku tani 118,262 zikibakia nchini kwa ajili ya wabanguaji wa ndani.

Mara kadhaa Serikali imekuwa ikieleza kuwa mpango wake ni kuwa na uzalishaji wa tani milioni moja kwa mwaka ifikapo msimu wa 2030/2031 huku ikilenga korosho zote zibanguliwe hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema msimu wa mwaka 2025/2027 matarajio ya mavuno ni tani 700,000 huku akisisitiza kuwa malengo ya tani milioni moja ifikapo mwaka 2030/2031 yako palepale.

Hata hivyo, ili kufikia malengo ya kubangua korosho yote, Katibu wa Chama cha Wabanguaji Wakubwa wa Korosho (TACP), John Nkundwanabake, amesema hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kufikia malengo hayo, ikiwemo kutoa vivutio kwa wabanguaji wa ndani ili kuongeza viwanda na uwezo wao wa kubangua.

“Kwa miaka mitatu iliyopita hali ya ubanguaji wa ndani inakua japo kasi ni ndogo ikilinganishwa na malengo. Tumetoka tani 6,000 hadi tani 24,000 sasa, na malengo ya Serikali ni kubangua tani milioni moja kwa miaka mitano ijayo. Hilo linawezekana kama uwekezaji katika ubanguaji utaongezeka,” amesema Nkundwanabake.

Amesema miongoni mwa vivutio vya kuongeza uwekezaji ni punguzo la tozo zinazotozwa katika zao hilo, lakini pia ufadhili au ruzuku katika mikopo ya wawekezaji katika eneo hilo ili kuwafanya kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuendesha shughuli zao.

“Uwezo wa juu wa viwanda vyote kubangua ni tani 103,000 lakini kwa sasa hakuna kiwanda kinachobangua ‘at full capacity’ (kwa utoshelevu), wengi ni asilimia 30 hadi 60. Jumla ya viwanda tulivyonavyo ni 57 lakini vinavyofanya kazi ni 36. Vingine vimesimama kwa kukosa malighafi na mtaji wa kuviendesha,” amesema Katibu huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Akros.

Amesema baada ya kufunguliwa kwa soko la awali ndipo nafuu ilipopatikana na ongezeko la ubanguaji likaonekana, lakini kwa kutoa vivutio zaidi, watafanya wabanguaji wa ndani kuweza kushindana katika mnada na wanunuzi wa nje huku malengo ya kuongeza thamani ya korosho yote yakifikiwa.

“Vivutio si tu vitaongeza uwezo wetu wa sasa, bali vitavutia wawekezaji wengine kuja kuwekeza katika eneo hilo. Kuuza korosho ghafi ni kuuza ajira, kwani kwa kila tani 5,000 kuna ajira zaidi ya 1,000 zinazalishwa. Hata mapato ya fedha za kigeni tunaweza kuyaongeza kwa zaidi ya asilimia 50 tukiuza korosho iliyobanguliwa,” amesema Nkundwanabake.

Amesema kwa kuuza nje zaidi ya tani 400,000 kuna zaidi ya ajira 90,000 zimepotea, hivyo anatamani kusikia Waziri wa Kilimo akitoa matumaini na mipango ya kukuza sekta hiyo kupitia bajeti inayotarajiwa.

Naye Mchambuzi wa Takwimu wa Kampuni ya Sabayi Investment, ambayo inamiliki kiwanda cha kubangua na kukamua mafuta ya korosho cha Tan-Ko, Happiness Kundi, amesema kiwanda chao kina uwezo wa kubangua tani 10,000 kwa mwaka, lakini sasa wanabangua tani 6,000 pekee.

“Sababu kubwa ni kutopatikana kwa malighafi, tunashindwa kushindana sokoni na wanunuzi wa nje. Lakini hata hivyo hali imekuwa afadhali baada ya kufunguliwa kwa soko la awali,” amesema Kundi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *