
Dar es Salaam. Msimamo wa ama kuendelea kugombea au kuweka rehani ndoto za kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu kwa makada wa Chadema, utajulikana kesho Alhamisi Aprili 3, 2025.
Kujulikana kwa msimamo huo, kutatokana na kikao cha watia nia wote wa ubunge pamoja na viongozi wakuu wa Chadema, kuhusu hatima ya nia zao za kutaka kuwania nafasi hizo.
Sababu ya kikao hicho na watia nia hao ni msimamo wa Chadema wa kutokuwa tayari kushiriki uchaguzi huo mpaka mabadiliko ya kisheria yatakapofanyika, ikiwa ni ajenda iliyopewa jina la ‘No Reforms, No Election.’
Kampeni ya ‘No Reforms, No Election’ ambayo imeanza kunadiwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa, ina lengo la kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi, ili mchakato uwe wa haki kwa vyama vyote.
Pia, vuguvugu la kunadi ‘No Reforms, No Election’ ili kuwajengea uwezo Watanzania kuhusu ajenda hiyo litahamia mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi kuanzia Aprili 4 hadi 10, likianzia wilayani Masasi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi inazo, tayari baadhi ya watia nia hao wamewasili jijini Dar es Salaam kuitikia wito huo ili kujua hatima ya kiu yao ya kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho na Taifa kwa ujumla.
Kikao hicho kitakachofanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, kitawahusu pia wanachama wote ambao walikuwa wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kama tangazo la Katibu Mkuu (John Mnyika), lilivyoelekeza.
“Kikao hiki ni cha muhimu sana na wahusika wote wahudhurie,”alisema Aman Golugwa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Chadema (Bara) katika waraka wake wa wito alioutoa Machi 24, 2025.
Sambamba na hilo, kikao hicho kinachoelezewa kuwa kitaanza saa nne asubuhi, kitajadili pia hali ya kisiasa na mwenendo wa Chadema katika kudai chaguzi huru na zenye kuaminika.
Licha ya Chadema kuja na No Reforms, No Election, lakini baadhi ya viongozi wakiwamo wa mikoa, hawajaielewa ajenda hiyo, wakisema inawaweka njia panda kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mmoja wa viongozi hao (jina limehifadhiwa) aliyewahi kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ameiambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 2, 2025 kuwa ajenda hiyo bado inaleta mkanganyiko miongoni mwao na inawaacha njia panda.
“Hata kesho kutaibuka mvutano kuhusu ajenda hiyo, kwa sababu tupo njia ya panda, miongoni mwetu tumeshajiandaa kwa takriban miaka mitano kuwania nafasi za uwakilishi wa wananchi.”
“Kuna wengine walishaanza maandalizi mbalimbali ikiwemo kwenda kwenye nyumba za ibada ili kupata uungwaji mkono, leo unamwambia eti No Reforms, No Election huyu mtu atakuelewa kweli,” amehoji kiongozi huyo.
Kwa mujibu wake, watekelezaji wa ajenda hiyo ni watia nia na chama ni mdhamini tu, kama hawajaielewa ajenda ni sawa na kuwaburuza na itakuwa vigumu kuitekeleza.
Mtia nia mwingine aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina amesema, “Nipo njia panda niende au nisiende, kwa sababu ajenda yenyewe inanipa mashaka na siielewi,” amesema.
Amesema viongozi wao wakuu wanapaswa kulitafakari hilo kwa kina na ikibidi, wawaache wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi waendelee mambo mengine yatafuata.
Maandalizi yamekamilika
Akizungumza na Mwananchi leo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema maandalizi ya kikao hicho yamekamilika na kitaanza saa tatu asubuhi.
“Maandalizi yapo vizuri na baadhi ya watia nia wameshawasili Dar es Salaam, wengine wanajiandaa kuja kushiriki kikao hiki muhimu kwetu,” amesema Rupia.