
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martine Mbwana amesema maduka kwenye mitaa iliyopo pembezoni mwa ghorofa lililoporomoka yatafunguliwa baada ya kuwatoa watu wote walionasa kwenye jengo hilo.
Tangu kutokea kwa ajali hiyo Kariakoo, Jumamosi ya Novemba 16, 2024, maduka kwenye baadhi ya mitaa yalizuiwa kufunguliwa.
Akitolea ufafanuzi hilo, Mbwana amesema jiografia ya Kariakoo imelazimu baadhi ya maduka yafungwe ili kutoa mwanya na mazingira rafiki ya uokozi.
“Kariakoo ni soko kubwa, wangesema kuruhusu kuna malori yanaingia huku isingekuwa sawa, hata hivyo baada ya kuhakikisha tumewatoa ndugu zetu wote walionasa kwenye kifusi, ile mitaa ambayo ipo pembezoni kidogo itaendelea na biashara,” amesema.
Akizungumzia usalama wa Kariakoo, Mbwana amesema,”hiki kilichotokea ni ajali, kila hatua inatukumbusha jambo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameunda timu ya watu 19 naamini itakuja na matokeo chanya.”
Kuhusu tathimini ya mali zilizoharibika, Mbwana amesema kuifahamu kwa sasa bado, kwa kuwa mbali na maduka katika jengo hilo pia kulikuwa na stoo.
“Kikubwa kwa sasa ni kuwaokoa ndugu zetu walionasa kisha mambo mengine yatafuata na kuhusu mmiliki hilo ni suala la polisi,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi