
Upo msemo maarufu kuwa, ’alivyo mzazi ndivyo alivyo mtoto’. Msemo huu ni mgumu kuubali hasa pale tunapozungumzia tabia mbaya tunazoziona kwa watoto.
Ingawa ni kweli yapo mazingira mengi yanayochangia kujenga imani, mtazamo na tabia ya mtoto, bado hatuwezi kupuuza nafasi kubwa aliyonayo mzazi kama mwalimu wa kwanza wa hisia za mtoto.
Ningependa tuangazie eneo moja la majeraha ya kihisia na kuona namna gani mzazi anapokuwa na majeraha hayo yasiyotibiwa ana uwezekano mkubwa wa kuleta madhara kwa kizazi chake.
Silengi kumfanya mzazi ajisikie hatia bali aone umuhimu wa kumlinda mtoto na kile kinachoendelea kwenye maisha yake.
Ukweli wa kisayansi tuliopata kuusema mara kadhaa kwenye safu hii ni kwamba hisia zina nguvu kubwa katika maisha yetu na kwamba mtoto anahitaji mwongozo wa karibu sana wa mlezi katika kujifunza namna ya kuzielewa, kuzimudu na kuzitumia kuboresha maisha yake na watu wanaomzunguka.
Kadhalika, ni ukweli wa kimaumbile kuwa watoto wana utegemezi mkubwa wa kihisia kwa wazazi.
Ikiwa haya matatu yana ukweli, nini kinatokea mzazi anapokuwa na majeraha ya kihisia? Je, unajuaje una majeraha ya kihisia?
Majeraha ya kihisia ni ile hali ya mtu kuwa na mvurugano wa kihisia unaotokana na mkusanyiko wa maumivu ya mengi aliyowahi kupita yanayomfanya ashindwe kuelewa hisia zake, kuwasilisha hisia zake, kujua athari ya hisia zake kwa wengine na hivyo, kwa namna fulani kujikuta anakuwa mtumwa wa hisia zake mwenyewe.
Mzazi anapokuwa na majeraha ya kihisia, mara nyingi hupata shida kuelewa hisia za mtoto wake. Ikiwa huwa unapata shida kuelewa mtoto anajisikiaje, hata anapokwambia jambo unakuwa mwepesi kulipuuza, na unapofanya hivyo unaamini hujakosea, unamkomaza mtoto na kadhalika, huenda unaishi na majeraha ya kihisia bila kujua.
Tukumbuke hitaji la msingi kwa mtoto, ukiacha chakula, ni hakikisho la dhati kutoka kwa wazazi kuwa hisia anazokuwa nazo zina maana, zinaeleweka na kwamba kuna mtu anayejali na kuzishughulikia.
Hili linapofanyika hujenga mazingira ya mtoto kujiona yuko usalama na hivyo, kama tuligusia wiki iliyopita, huwa na uhuru wa kudadisi na kujifunza zaidi.
Mazingira yanayomfanya mtoto aone hisia zake si kitu cha maana, aghalabu humfanya aanze kujisikia kupuuzwa, kutokueleweka na hatimaye kuanza kujenga dhana kuwa hakuna mtu anayemuelewa.
Kingine ni kushindwa kumpenda mtoto sawa sawa. Kuna kisa kimoja nakikumbuka kwenye kitabu cha What Happened to You? kilichoandikwa na Bruce Perry na Oprah Winfrey. Mama mmoja aliyeathirika na unyanyasaji wa kijinsia akiwa mtoto alijikuta akipata ugumu kutoa upendo kwa mtoto wake, licha ya mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwake.
Mama huyu aiishi kwa hofu na wasiwasi, akijiona kama mtu asiyeweza kutoa kile anachojua mtoto wake anahitaji. Unaweza kuona majeraha ya kihisia ya mzazi yanavyoweza kuathiri uhusiano wa familia, ambapo mzazi anakosa namna ya kushughulikia mahitaji ya kihisia ya mtoto.
Bruce Perry anatoa mfano wa mtoto aliyeishi na baba aliyekuwa na huzuni kubwa kutokana na kupoteza mkewe.
Baba huyu alishindwa kutoa upendo wa kihisia kwa mtoto wake, na mtoto alijikuta akikosa usalama kihisia na alikuwa na shida za kujieleza kihisia.
Hii ilimfanya mtoto kuwa na shida za kujiamini na kutokuwa na uwezo wa kushughulikia vikwazo vya kihisia alivyokutana navyo katika maisha yake.
Madhara ya majeraha ya kihisia ya wazazi yanaweza kutengeneza mzunguko mbaya wa kihisia unaovuka kizazi na kizazi.
Mtoto aliyeishi na mzazi asiyejali hisia zake, naye akiwa mzazi, anakuwa na ugumu wa kutoa upendo kwa watoto wake. Inakuwa kama kujenga kizazi kingine kinachorudia yale yale ya kizazi kilichopita.
Tuhitimishe na habari njema. Uwezekano wa kubadili hali hii upo. Tunaweza, kwa mfano, kujifunza mbinu rahisi ya mazungumzo yanayotuunganisha na mtoto kihisia. Hapa tunamaanisha kujfunza kutoa jibu linalofaa kwa mtoto hata kama unajisikia vibaya na ungerahisisha kwa kupuuza.
Katika mazingira ambayo unapata shida kujieleza kihisia, mahali pa kuanzia ni kutenga muda wa kutosha kuwa na watoto hata kama huna mengi ya kuzungumza nao. Upatikanaji wako una manufaa makubwa wakati mwingine kuliko hata maneno.
Upo umuhimu wa kuelewa historia yako ya kihisia kama mzazi na ukaazimia kutokuhamishia majeraha hayo kwa mtoto. Unapoona unapata shida kuelezea hisia zako, pengine hiyo ni muhimu kutafuta msaada wa kitaalamu.