Hata Uholanzi, Canada na Uswisi zasema zitamkamata Netanyahu akithubutu kwenda katika nchi zao

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi amekaribisha uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wa kutoa hati ya kukamatwa Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kwamba iwapo ataingia Uholanzi atatiwa nguvuni.

Caspar Veldkamp amesisitiza kuwa nchi hiyo haitafanya tena mawasiliano na Netanyahu wala waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant, ambao Mahakama ya ICC imeamuru wakamatwe kwa kuhusika na jinai za vita na jinai dhidi ya binadamu.

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema: “ni muhimu sana kwamba kila mtu azingatie sheria za kimataifa” na akaongeza kuwa nchi yake itatii maamuzi ya mahakama za kimataifa.

Katika upande mwingine, Ofisi ya Sheria ya Shirikisho la Uswisi imesema inalazimika kushirikiana na ICC chini ya Mkataba wa Roma na kwa hivyo italazimika kumkamata Netanyahu na Gallant endapo wataingia nchini humo na kuanzisha utaratibu wa kuwakabidhi kwa mahakama hiyo.

Serikali ya Afrika Kusini imetoa taarifa ikikaribisha uamuzi wa ICC na kusema ni “hatua muhimu kuelekea kupatikana haki kwa uhalifu uliofanywa dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita huko Palestina”.

Harakati za Hamas na Jihadul-Islami pamoja na Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, nazo pia zimekaribisha uamuzi wa Mahakama ya ICC…/