Hata Bongo tunaweza kuiga hilo kwa Whitney Houston

Dar es Salaam. Hapo Januari 19, 2021, mkongwe wa miondoko ya Country Music, Dolly Parton alitimiza umri wa miaka 75, msanii mwenzake Whitney Houston alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumtakia heri ya kuzaliwa na maisha mazuri.

Ikiwa ni miaka 13 imepita tangu kutokea kwa kifo cha Whitney, Malkia wa Soul, RnB na Pop, bado kurasa zake za mitandao ya kijamii zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kitu ambacho ni tofauti kabisa na wasanii wa Tanzania na hata barani Afrika.

Ikumbukwe Whitney alifariki Februari 11, 2012 katika hoteli ya Beverly Hills huko Los Angeles, Marekani akiwa na umri wa miaka 48, huku matumizi ya kupinduzi ya dawa za kulevya yakitajwa kusababisha kifo chake.

Dolly Partorn ndiye aliyeandika wimbo ‘I Will Always Love You’ na kuurekodi mwaka 1973, baadaye 1992, Whitney Houston alikuja kuurudia ambapo ulitumia kama soundtrack ya filamu yake, The Bodyguard.

Toleo hili la Whitney ndilo maarufu zaidi, ulifanya vizuri ukishika namba moja chati za Billboard Hot 100 kwa wiki 14, ukishinda tuzo mbili za Grammy 1994 na hadi sasa unatambulika kama wimbo uliouza zaidi duniani kwa muda wote.

Mafanikio hayo yaikaibua minong’ono ya chuki kati yao, kwamba Dolly Partorn aliona wivu wimbo aliouandika yeye kwenda kumpa mafanikio makubwa mtu mwingine, lakini hadi sasa wanaonyeshana upendo ingawa mmoja katangulia mbele za haki.

Ni wazi mitandao hiyo ya kijamii ya Whitney inaendelea kusimamiwa na watu ambao walikuwa wanafanya hivyo au waliyokuja kupewa shughuli hiyo na menejimenti ya msanii huyo.

Huu umekuwa utaratibu wa watu maarufu duniani katika muziki, michezo na filamu lakini kwa hapa Tanzania mambo ni tofauti kabisa.

Baadhi ya watumiaji wa mtandao wa X, zamani Twitter nchini walipatwa na mshangao na kuwa na maswali mengi baada ya ukurasa wa rapa Godzilla kuchapisha ujumbe ukiwauliwa mashabiki kama wapo tayari wa ujio nyimbo zake mpya.

Katika ulimwengu wa sasa ambao mitandao ya kijamii imekuwa na nguvu kubwa, wasanii waliotangulia mbele za haki kurasa zao huendelea kutoa taarifa za kazi walizozifanya kipindi cha uhai wao kama sehemu ya kuwaenzi na kueneza uelewa zaidi kuwahusu wao.

Tanzania imejaliwa kuwa vipaji vingi ambavyo kwa sasa havipo dunia, nchi hii imenufanika na uwepo wa Bi Kidude, King Majuto, Remmy Ongala, King Kiki, Steven Kanumba, Ngwea, Langa n.k.

Basi menejimenti zao ziinge jambo hilo kwa ile ya Whitney Houston, zifungue kurasa rasmi za mitandao ya kijamii kama sehemu ya kuwapa maua yao na kuendelea kuilinda alama waliyoicha kupitia sanaa yao ambayo bado ina nguvu ya ushawishi katika jamii.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *