Hat trick yampa mzuka Mukwala Dabi ya Kariakoo

NYOTA wa kimataifa wa Uganda, Steven Mukwala ameongeza hamasa kwa upande wa timu ya Simba kabla ya pambano la Dabi ya Kariakoo litakalopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabao matatu aliyofungwa nyota huyo wa Simba dhidi ya Coastal Union katika mechi iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, imemfanya Mukwala kuonekana kama aliyeibeba Dabi kiwa upande wa Mnyama anayepambana kujivua unyonge mbele ya Yanga.

Ushindi wa jana umeiongezea Simba mzuka kwani imeifanya ifikishe pointi 54 baada ya mechi 21, ikiwa nyuma ya Yanga inayoongoza kwa sasa ikiwa na pointi 58 baada ya mechi 22 ilizocheza ikiwa pia ndio watetezi wa taji la Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo kwa sasa.

Mukwala amesema kwa sasa nguvu zote anazielekeza katika mchezo dhidi ya Yanga ambayo ni muhimu kwa timu yake kushinda ili kutengeneza nafasi ya kukaa kileleni na kusogelea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Kazi yangu ni kupambana kwa kushirikiana na wenzangu kutimiza malengo ya timu ambayo ni kushinda kila mchezo uliopo mbele yetu,” amesema Mukwala.

Nyota huyo mwenye mabao manane kama aliyonayo Leonel Ateba aliyepo pia Simba, ameongeza kuwa anatambua mchezo utakuwa mgumu lakini kama alivyowafanya Wagosi wa Kaya basi moto huo huo pia ataenda kuwachoma nao Wananchi na kuvunja ile rekodi ya Simba kucheza mechi nne mfululizo dhidi ya Yanga bila kupata ushindi.

“Mashabiki waje wajitokeze kwa wingi uwanjani timu yao ni nzuri na wachezaji tunapambana kuwafurahisha hivyo wasiwe na wasiwasi hata kidogo,” amesema Mukwala.

Kuhusu kuwania kiatu cha ufungaji bora sasa akiwa na mabao manane, akizidiwa mawili na vinara Clement Mzize, Prince Dube wote wa Yanga na Jeah Charles Ahoua wa Simba wenye 10 kila mmoja, wakifuatiwa na Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye mabao tisa kwa sasa.

Mukwala amesema kwa sasa ana timiza malengo ya timu kushinda kila mchezo ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa kwa kushirikiana na wachezaji wenzake alafu ndio malengo yake kuona mwisho wa msimu amefunga magoli mangapi ambayo yamemweka kwenye nafasi gani.

Simba na Yanga zinakutana katika pambano hilo la marudiano kwa msimu huu, baada ya awali kukutana Oktoba 19 mwaka jana na Yanga kushinda 1-0 kwa bao la kujifunga la beki wa Simba, Kelvin Kijili likiwa ni pambano la 113 kwa timu hizo kukutana tangu 1965 hadi mwaka jana.