
Dar es Salaam. ‘Anko’ Hashim Lundenga. Wazo lake la Miss Tanzania alizalisha nyota wengi wa kike ambao kupitia shindano hilo maisha yao yalibadilika kabisa. Hapo ndipo utaona namna Anko Lundenga alivyoacha alama. Pumzika Lunde.
1994 alikuwa kijana tu wa miaka 37. Mtoto wa mjini kweli kweli. Wenyeji wakamuita ‘Anko Lunde’. Fundi wa maneno. Kabla ya uwepo wa viumbe kama Ruge. Lunde alikuwa miongoni mwa watu waliojaaliwa akili ya pesa ya burudani.
Kuna Simba na Yanga. Msondo na Sikinde. Kulikuwa na tamasha moja tu nchi hii. Nalo ni shindano la Miss Tz. Kabla ya Fiesta na Summer Jam. Na kabla ya Likizo Time na Mziki Mnene na Wasafi Festival. Ilikuwa noma.
Aina Maeda ndiye Miss Tanzania wa mwaka 1994. Mwaka mmoja kabla ya utawala wa Mkapa. Tayari Lundenga alianza kutengeneza mastaa wa kike katika taifa hili. Baada ya lile la 1967 lililomtoa Theresa Shayo.
1995 ‘Anko’ akatuletea Emily Adolf. Kiumbe bora wa kike kutoka mitaa ya Dodoma. Aliwavuruga warembo wa Daslama na kutwaa taji la Miss Tz kindava. Emily alisimama wima kama noti mpya ya Mmarekani.
Sura, ngozi, umbo, lugha na uwezo wa kujieleza. Na akili kubwa maana unaweza kujua lugha lakini akili sifuri.
Aina na Emily sijui wako wapi kwa sasa. Lakini sihitaji ushahidi wa DPP kujua kuwa wana maisha mazuri.
Hawakushiriki Miss Tz ili baadaye waigize Bongo Movie. Wengi wao kidato kilipanda kichwani kabla ya kupanda jukwaa la Miss Tz. Warembo wa nyakati zile walikuwa mtambuka kiakili. Unakuaje Miss Tz usiyejua kitu?
Shose Sinare ndiye Miss Tz wa 1996.Miongoni mwa warembo bora kupata kutokea nchi hii. Jukwaa liliheshimu hatua zake. Majaji walipigwa ganzi. Na watu ukumbini walitikisa vichwa. Siyo kwa kupinga bali kukubaliana naye kuwa anastahili.
Shose Sinare kabla ya matatizo ya kesi. Alikuwa ni mmoja wa maofisa wa Stanbic Bank. Miss Tz ya wakati ule haikuzalisha waigizaji wa filamu. Ilizalisha warembo walio elimika na wenye upeo mkubwa.
Mikoa ya Kaskazini kuna totozi sana. 1997 Lundenga akatuletea mrembo Saida Kessy kutoka Arusha. Akawa Miss Tanzania. Basila Mwanukuzi kutoka Kino akawa Miss Tz 1998. Ni miongoni mwa pisi kali zilizoandikwa sana.
1999 Kaskazini wakateka tena shindano na taji kuvalishwa mwanadada Hoyce Temu. Ukiwafuatilia utaelewa kuwa Miss Tz ile ilikuwa moto. Hoyce ni Mh. Balozi kwa sasa. Noma sana!
Jackline Ntuyabaliwe kutokea Ilala, akarudisha heshima ya Daslama mjini. Akapokea taji kwa Hoyce Temu mwaka 2000.
Huyu K-Lynn mwenye watoto pacha wenye ‘fyucha’ ndefu.
Happiness Magesse, anatambulika kimitindo kama Millen. Mnyenyekevu. Mkimya. Mrefu. Akaendeleza heshima ya warembo wa Dar. Akabeba taji la Miss Tz 2001. Nyakati hizi Lundenga alikuwa juu kama Mlima Kilimanjaro.
2002 ikawa tena kwa Dar. Kiumbe mmoja sahihi sana kwa kila kitu. Na mwenye sura tulivu muda wote kama yuko kizimbani. Angela Damas akawa Miss Tz wetu. Anko Lunde alituleta huyu mrembo mwenye ngozi ‘miksa’.
Dar tena. 2003 totozi kutoka ‘TMK’ Sylvia Bahame. Akachukua pointi zote tatu. Mwanya wake, ungeweza kabisa kuhamisha karakana ya mwendokasi pale Jangwani. Na mafuriko yakaisha kabisa. Pisi ya maana.
2004 Daslama wakaendeleza ubabe. Faraja Kotta (Nyalandu). Mtoto wa kishua kutoka ‘Obei’. Lips takatifu na ngozi iliyotakaswa. Hakuchukua taji tu, bali taji na zawadi ya gari la thamani kubwa sana. Mtoto akawa ‘anapushi’ ndinga ya maana.
Ili ujue kuwa nyakati hizo washiriki wa Miss Tz hawakuwa poapoa. Kaulize Mzee Kota ni nani nchi hii? Utaelewa kuwa walioshiriki Miss Tz nyakati hizo ni wasomi au watoto f’lan wa kishua vilevile. Hawakushiriki ili wakafungue bar.
Nancy Sumari. Mtoto wa Kiarusha. Mzuri kwa vigezo halisi vya uzuri sana. Hata ukimshitukiza asubuhi akiamka au akiwa msibani. Bado utagundua umekutana na msichana mrembo sana. Mzuri wa sura na rangi.
Mzuri wa akili na kujieleza. Alifunga ndoa na kiingereza. Na zaidi mtamu wa sauti. Kama asingeshinda taji la mwaka 2005. Majaji wote wangezikwa siku ya pili yake baada ya shindano. Wazungu wa Miss World pia walimuelewa sana.
Nao walikubaliana kuwa Nancy awe mrembo bora wa Afrika. Hii maana yake ni kwamba majaji wa Miss Tz walikuwa sahihi kabisa. Nancy ni wale warembo unaweza kuuliza, kama hii ni damu yetu kweli au Barbados?
Kubwa la maadui. Mama la mamaake. Wema Abraham Sepetu. Akapindua meza pale Diamond Jubilee. Vuruga akili za majaji. Mtoto kaenda hewani, anapiga ngeli, anatema mayai. Lips zimetuna f’lan kama kile kilima cha Masaki.
Hakuna aliyetaka kutazama urembo wa Jokate. Hakuna aliyemuona Irene Uwoya. Hakuna aliyepoteza muda na Lisa Jensen. Kila mtu alimuona Wema Sepetu tu. Shindano kubwa lililokuwa na ushindani mkubwa na ubishani mubwa.
Nani zaidi Wema na Jokate. Mpaka hii leo ingawa siyo rasmi. Bado kuna hali f’lani usiojipambanua wazi kwa Jokate na Wema. Na kuanzia hapo Miss Tz ikapoteza muelekeo kabisa. Hakuna mwaka ambao Miss Tz itengeneza mastaa wengi kama 2006.
Kutoka 1994 mpaka 2006 ni miaka 13. Hii ndiyo miaka ambayo Miss Tz ilizalisha wasichana ambao baadaye wakageuka kuwa almasi mchangani. Baada ya 2006, Miss Tz halikuwa ni shindano tena bali tafrija. Ndo ukweli.
Asante Hashim Lundenga ‘Anko’. Ni kweli kwamba uliutumia sahihi muda wako ukiwa hai. Kuna maelfu ya watu umewapa maisha huku duniani. Mpe salamu nyingi sana Amina Mongi. Na hakika mbele yako nyuma yetu.