Dar es Salaam. Hatimaye rekodi lebo ya Konde Music Worldwide yake Harmonize imeridhia msanii wake wa pekee na wa kwanza kumsaini, Ibraah kuondoka baada ya kufanya kazi pamoja ya kutoa burudani kwa mashabiki kwa takribani miaka mitano.
Tunaweza kusema hatua hii muhimu ni mwisho au mwanzo za zamani nyingine ndani Konde Music ila haiondoi ukweli kwamba hadi hapa tulipofika, kuna eneo Harmonize hana deni kwa wasanii wote waliopita katika lebo hiyo.

Baada ya sakata la Ibraah kuomba kuondoka katika lebo hiyo kufika mbele ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata) ili kupata usuluhishi, Harmonize ameibuka na kusema haina haja ya kufika huko kwa msanii aliyemtoa yeye, hivyo anamtakia kila la heri.
Ikumbukwe Ibraah alitambulishwa Konde Music mnamo Aprili 2020 akiwa ndiye msanii wa kwanza kisha wakafuata wengine watano ambazo ni Country Wizzy, Cheed, Killy, Anjella na Young Skales kutokea Nigeria.
Harmonize alitangaza rasmi kuanzisha lebo ya Konde Music hapo Oktoba 10, 2019 ikiwa ni kipindi kifupi baada ya kujitoa katika lebo ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambayo ilimtoa kimuziki kupitia wimbo wake, Aiyola (2015).
Tunasema hana deni kwa sababu wasanii wote saba waliowasaini Konde Music kashirikiana nao na nyimbo walizotoa zimefanya vizuri, na hiki ndicho wanakifuata wasanii wengi katika lebo za wasanii wakubwa wakiamini ushawishi wa bosi wao kimuziki utawasaidia.
Tangu amejiunga Konde Music mwaka 2020, kila mwaka Ibraah alikuwa anatoa wimbo na Harmonize, tayari wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni One Night Stand (2020), Addiction (2021), Mdomo (2022), Tunapendeza (2023) na Dharua (2024).

Kolabo yao ya kwanza na ya mwisho, ndizo zimefanya vizuri zaidi, hadi sasa video ya wimbo, One Night Stand (2020) imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 22, huku Dharua (2024) ikitazamwa mara milioni 21 ndani ya mwaka mmoja.
Inaelezwa kuwa Harmonize alimkuta Ibraah amesharekodi wimbo, One Night Stand (2020) akaupenda na kuomba kuongeza vesi yake kitu ambacho Ibraah alikubali na ulipotoka ukafanya vizuri na kumtambulisha zaidi.
Kwa ujumla chini ya Konde Music, Ibraah ametoa EP tatu, Steps (2020), Karata 3 (2021) na Air Piano (2024) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022) ambayo haikushirikisha msanii yeyote wa lebo hiyo.
Msanii mwingine aliyebebwa sana na kolabo za Harmonize pale Konde Music ni Anjella, wawili hao wameshirikiana kwenye nyimbo tano ambazo ni All Night (2021), Kama (2021), What Do You Miss (2021), Kioo (2022) na Toroka (2022).

Video ya wimbo, Kioo (2022) imetazamwa zaidi ya mara milioni 9.9 You Tube na ndio video pekee ya Anjella ambayo imepata namba kubwa zaidi katika mtandao huo unaotumika na mashabiki wengi wa muziki nchini.
Na Anjella ndiye msanii pekee wa kike aliyeshirikishwa katika albamu ya pili ya Harmonize, High School (2021), hii ni tofauti na albamu ya kwanza, Afro East (2020) ambayo ilishirikisha wasanii wawili tu wa kike, Lady Jaydee na Yemi Alade.
Kwa upande wake Country Wizzy, kabla ya kujiunga na Konde Music, tayari alishasikika katika wimbo wa Harmonize, Bedroom Remix (2020) ambao ulikutanisha wasanii wengine kama Darassa, Billnass, Nay wa Mitego, Moni Centrozone, Rosa Ree n.k.
Baada ya kusaini Konde Music, Country Wizzy alitokea katika video ya wimbo wa Harmonize, Jeshi (2020), huku naye Harmonize akitokea katika video ya ngoma ya Country Wizzy, Intro (2020) iliyomtambulisha katika lebo hiyo.
Muda mfupi uliofuatia, wawili hao wakatoa wimbo uliofanya vizuri sana, Far (2020) ambao hadi sasa video yake ndio namba moja kwa kutazamwa zaidi YouTube kwa Country Wizzy, rapa aliyefunika na albamu yake, Yule Boy (2019) yenye nyimbo 30.
Ikumbukwe baada ya Country Wizzy kuachana na Konde Music hapo Januari 2022, alienda kuanzisha lebo yake, I Am Music ambayo ilikuja kulisaini kundi la Hip Hop, Fresh Boys lenye wasanii wanne.
Nao Cheed na Killy ambao walijiunga na Konde Music baada ya kujitoa Kings Music yake Alikiba, licha ya kazi zao kuchelewa kutoka, hawakuondoka mikono mitupu katika lebo hiyo kwani kila mmoja alitoa EP na zote Harmonize alishiriki.
Cheed alitoa EP yake, Endless Love (2022) yenye nyimbo sita huku Harmonize akishiriki katika wimbo ‘Konkodi’ ila kwa bahati mbaya hadi Cheed anaondoka Konde Music kufuatia mkataba wake kusitishwa, video ya wimbo huo ilikuwa haijatoka.
Naye Killy alitoa EP, The Green Light (2020) yenye nyimbo sita pia huku Harmonize akisikika katika wimbo ‘Ni Wewe’ ambao video yake imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 21 ikishika namba moja kwa msanii huyo.
Tukija kwa Young Skales wa Nigeria, huyo kabla ya kujiunga na familia ya Konde Music, alishafanya kolabo kadhaa na Harmonize kama Fire Waist (2018), Oyoyo (2019), Oliver Twist II Remix (2020) n.k.
Kwa muktadha huo, Harmonize anaweza kuhukumiwa kwa mambo mengine kama ya kiutendeji ndani ya Konde Music Worldwide lakini linapokuja suala la muziki, hana deni upande huo, alijitoa kikamilifu kwa kila aliyemsaini na sasa amebaki pekee yake.