Dar es Salaam. Mwanamuziki Harmonize amekanusha kauli ya aliyekuwa msanii wake Ibraah ya kumdai kiasi cha Sh1 bilioni, ili aweze kutoka lebo ya ‘Konde Gang’.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Harmonize ametoa maelezo kuhusu sakata hilo huku akiweka wazi kutofahamu andiko la Ibraah katika mitandao ya kijamii la kumdai Sh1 bilioni.
“Niko hapa kiadress jambo linalomuhusu mdogo wangu Chinga. Kwanza kabisa nikiri alinitumia meseji na kuniomba kwamba anataka kuondoka kwenye lebo akawe Independent Artist nilimkubali na kumtakia kila la kheri nikamwambia kaa chini na viongozi wa Konde Gang muone mnafanyaje.

“Mkataba wake unasema endapo anataka kuondoka na kununua haki miliki zake za nyimbo alizozifanya hata zile alizozifanya na mimi, ili ziwe za kwake muda wote, ziingize pesa kwake inatakiwa alipie kuzinunua. Hicho kiasi cha pesa kilichotajwa kwenye mkataba ambao alisaini miaka minne iliyopita na kampuni ya Konde Music,”amesema Harmonize
Afunguka kuhusu kumdai Sh1 bilioni
“Sijui nini kimetokea kwake baadaye akaja kusema kwenye social media kwamba nimemdai kiasi cha Sh1 bilioni nikiri kwamba sijamdai pesa hiyo. Nisingependa tena pesa yangu ije kunichafua mimi mwenyewe. Kwa sasa ni msanii huru namtakia kila la kheri promota mkiwa na show muiteni apate riziki aisaidie familia yake,” amesema Konde Boy
Aidha akizungumza kuhisiana na ishu ya BASATA kutoitikia wito huo, ameeleza kuwa aliliwasilisha kwa menejimenti yake ili imuwakilishe.
“Lakini pia kuhusiana na Basata nilipata wito na niliomba menejimenti yangu iniwakilishe nilitaka kujua tatizo nini, kwa sababu mazungumzo yangu na Bwana Chinga sikutegemea yangeweza kufika Basata.
“Viongozi wa Basata wanapataje muafaka lakini wakanambia waliyonambia so far nisingeweza kuyashare sasa hivi. Mimi sikuona haja ya kusuluhisha na mdogo wangu au msanii ambaye nimemtengeneza mimi mwenyewe sikuona haja ya kutengeneza sitofahamu na tahaluki,”amesema Konde Boy
Aidha ameongezea kwa kusema “Nimemruhusu aende akafanye mziki wake and make sure mnamsapoti pia. Na kuhusu kauli yake ya nimemuita chumbani it’s sad na sio kwamba sijui kuna baadhi ya watu wanaweza kuamini kwamba ni kweli lakini sina namna kwa sababu mtoto akiunyea mkono huwezi kuukata.

“Kwanza nimemuachia Mungu, pili nimemsamehe na mwisho namuombea mimi sihitaji msamaha wowote kutoka kwake akiona kuna haja ya kuomba msamaha ni sawa akiona hakuna haja pia ni sawa,”amemalizia Harmonize