Hapa kwenye ukuta Simba SC, Yanga watauana

JOTO limepanda kati ya Yanga dhidi ya Simba, mchezo unaopigwa leo pale Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Timu zote zinatokea kambini zilikokuwa zikifanya maandalizi ya mwisho kabla ya kumaliza msimu upande wa ligi ukiwa mchezo wa pili baina yao.

Msimu huu timu hizo kila moja imekuwa na ubora wake kwenye safu ya ulinzi zikijigawanya kwenye makundi tofauti lakini Simba kujiweka kwenye ubora zaidi kabla ya kwenda kukutana hii leo.

DABI 02

Simba ukuta mzito

Ukipima ni ukuta upi umeruhusu mabao machache, basi utaitaja haraka Simba ambayo mpaka inakwenda kukutana na Yanga ikiwa imeruhusu mabao manane, ikiwa na ndicho kikosi kilichoruhusu machache zaidi.

Nyuma ya Simba ipo Yanga ambayo imewazidi Wekundu hao kwa bao moja pekee ikiruhusu mabao tisa ikiwa ndio timu ya pili iliyoruhusu nyavu zake kutikiswa mara chache zaidi.

Eneo hilo linatoa sura ya ubora kwamba, Simba inaonekana kuwa na ukuta imara kuwashinda watani wake Yanga, lakini ikumbukwe Wekundu hao wana kiporo cha mchezo mmoja ambao haukuchezwa dhidi ya Dodoma Jiji.

DABI 01

Mabeki Yanga vinara kufunga

Ukija eneo la ukuta upi umekuwa ukifanya kazi zaidi ya kufunga, hapo utaitanguliza Yanga ambayo mabeki wake licha ya kuzuia wanashiriki kiuhalisia kutengeneza ushindi wa timu.

Lakini, pamoja na mabeki ya Yanga kuwa vinara wa kufunga dhidi ya wale wa Simba, pia mabeki wa timu zote mbili wamegongana kwenye ufungaji, ukiacha jukumu lao la kuzuia ambapo wamekuwa wakishiriki kutengeneza ushindi kwa timu.

Mabeki wa Simba kinara wa kufunga mabao ni beki yule wa kulia, Shomari Kapombe mwenye mabao matatu akifuatiwa na beki wa kati, Che Malone Fondoh aliyefunga mara mbili kisha nahodha wao Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Abdulrazak Hamza wakifunga moja moja. Yanga ukuta wake una watu wanaojua kufunga ukiongozwa na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ anayeongoza kwa ufungaji kwa mabeki akiwa na mabao manne ambapo nyuma yake kuna Israel Mwenda na Chadrack Boka ambao kila mmoja kafunga moja moja.

DABI 04

Simba pasi za mabao

Kazi nyingine ya mabeki wa pembeni ni kupika mashambulizi na Simba wameendelea kuwa juu kwa kutoa jumla ya asisti 10.

Vinara wa asisti kwenye ukuta wa Simba wamefungana mabeki watatu – Kapombe, Tshabalala na chaguo la pili nyuma ya nahodha huyo Valentin Nouma ambao kila mmoja ana asisti tatu kisha David Kameta ‘Duchu’ mwenye moja.

Yanga ukuta wake bado haujatengeneza asisti nyingi ukiwa nazo nne kutokana na timu kutengeneza mashambulizi mengi kutokea katikati ambapo mabeki waliotengeneza asisti hizo ni Boka mwenye mbili akifuatiwa na Mwenda na Kibwana Shomari ambao kila mmoja ametengeneza moja.

Diarra, Camara

Timu hizo zitaingia kwenye dabi ya tatu msimu huu kila moja ikiwakilishwa na kipa wa kigeni ambapo ukiwauliza mashabiki wa Yanga nani atadaka, jibu litakuwa rahisi – Djigui Diarra na swali kama hilo likienda kwa Simba watakutajia Moussa Camara.

Makipa hao wamekuwa na mchango kwenye ufanisi wa kuta zao ambapo Camara amekuwa kinara wa ‘klinishiti’ akiwa nazo 15 ndani ya michezo 20 aliyocheza, wakati Diarra anazo 11 kwenye mechi 16 alizocheza.

Diarra ndani ya mechi 16 ameruhusu mabao saba akiwa ndiye kipa aliyeruhusu machache zaidi akifuatiwa na Camara aliyeruhusu mabao manane.