Hamza afichua siri Zanzibar, Kibu atajwa

KIKOSI cha Simba kinashuka uwanjani kesho Jumapili kukabiliana na Stellenbosch ya Afrika Kusini, huku mastaa wa timu hiyo wakiongozwa na beki wa kati, Abdulrazack Hamza, wakitoa kauli ya kibabe.

Simba imetinga hatua hiyo baada ya kuing’oa kwa penalti 4-1 Al Masry ya Misri waliyotoka nayo sare ya mabao 2-2 matokeo ya jumla kila timu ikishinda nyumbani 2-0, na kesho zitavaana katika mchezo wa mkondo wa kwanza kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Hamza anayekipiga Simba kwa msimu wa kwanza akisajiliwa kutoka Sauzi, akizungumza kwa niaba ya mastaa wenzake, alisema ni heshima kubwa kwa wachezaji na Wanasimba kutinga nusu fainali, lakini anaamini kama watakaza buti wanaweza kufika mbali zaidi na kuweka historia itakayodumu muda mrefu klabuni na katika vitabu vya soka.

Beki huyo tegemeo katika ukuta wa Simba akishirikiana na Che Fondoh Malone ambaye ni majeruhi, Chamou Karaboue sambamba na kipa Moussa Camara ‘Spider’, aliliambia Mwanaspoti kuwa mechi ya robo fainali imethibitisha ubora wa viwango vya wachezaji wa kikosi hicho katika michuano hiyo ya CAF.

Alisema kama wachezaji wanatambua kila hatua inakuwa na ushindani mkali, hivyo wanazidi kuongeza bidii katika mazoezi ili kulinda viwango kwa ajili ya kuhakikisha wanafika mbali na ikiwezekana ubingwa wa Afrika waubebe ikiwa ni klabu ya kwanza ya Tanzania. “Niseme wazi hii ni heshima kubwa kufika hapa. Kinachotusaidia kucheza vizuri ni ushindani wa namba baina ya wachezaji wenyewe kwa wenyewe, hivyo kila mmoja anakuwa anajituma kuhakikisha anafanya kitu kitakachokuwa msaada kwa timu,” alisema Hamza.

“Bado hii haiwezi kuwa ndio mwisho wetu, tunapaswa kupambana zaidi katika mechi ya nyumbani na ugenini za hatua hii ili tuvuke na kwenda fainali, kwani bado tunaiona nafasi hiyo ipo kwa Simba.” Tangu Hamza ajiunge na Simba, Julai 4,2024, akitokea SuperSport ya Afrika Kusini, amekuwa chaguo la kwanza la kocha Fadlu Davids kutokana na kiwango bora ambacho kinazungumzwa hadi na wachezaji wenzake akiwemo Kibu Denis.

Kibu alinukuliwa na Mwanaspoti akisema Hamza anavyomkaba mazoezini ni kipimo kizuri kwake binafsi kinachotafsiri kile anachofanya katika mechi za mashindano. Rekodi zinaonyesha katika Ligi Kuu, Simba imecheza mechi 22 na kati ya hizo, Hamza amekosa tano, kwani amezicheza 17 akitumia dakika 1473, huku akifunga bao moja, jambo ambalo linaonyesha umuhimu wake katika kikosi.

Simba ndio yenye ukuta mgumu kufungika kwani imeruhusu mabao manane katika mechi hizo na katika michuano ya CAF msimu huu imefungwa mabao saba kupitia mechi 10, zikiwamo mbili za raundi ya pili, sita za makundi na mbili robo fainali ilhali yenyewe ikifunga 13.

“Ninachoamini mafanikio ya timu ndio ya wachezaji, jambo la msingi kila ninapopata nafasi ya kucheza ni kwa malengo ya timu mengine yanafuata baadaye,” alisisitiza Hamza aliyewahi kukipiga Mbeya City, KMC, Namungo kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa SuperSport ya Sauzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *