Hamisa Mobetto siyo urembo tu, na huku yupo vizuri

Dar es Salaam. Ukiachilia mbali Hamisa Mobetto kuwa mwanamitindo, mjasiriamali na muhamasishaji,  amepitia mambo mengi tangu alipoanza safari ya umaarufu.

Hamisa Mobetto kwa zaidi ya miaka saba amefanya vizuri kwenye kiwanda cha urembo yaani kuanzia mwaka 2011 ambapo alishiriki Miss Indian Ocean alipokuwa mshindi wa tatu na kufanikiwa kushiriki Miss Tanzania mwaka huohuo. 

Mwaka 2012 alishiriki Miss University na kufanikiwa kuwa miongoni 10  waliofanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Mnamo 2018, alishinda na kuwa Mwanamitindo wa Kike wa Mwaka katika Tuzo za Swahili Fashion Week. Lakini pia mwaka huohuo aliteuliwa kuwa muongozaji wa shindano la Urembo la Miss Tanzania na pia aliteuliwa kuwa Mjasiriamali Bora Mwanamke wa Afrika Mashariki katika Tuzo za BEFFTA.

Desemba 2020, alishinda tuzo ya Mwanamitindo Bora wa Kike wa Kidijitali wa Mwaka katika Tuzo za Kidijitali Tanzania.

Maisha na Muziki

Licha ya kufanya vizuri muda mrefu kwenye urembo Hamisa amewahi kujihusisha na muziki wa Bongo Fleva ambapo aliachia ngoma kadhaa. 

Mwaka 2017, Hamisa alionekana kwenye video ya Diamond Platnumz, kwenye wimbo wa ‘Salome’ ambao alitokea kama video vixen. Video ya wimbo huo ilifanikiwa kupokelewa kwa ukubwa kutokana na uhusika aliotokea nao mrembo huo.

Mnamo 2018, alitoa wimbo wake wa kwanza ‘Madam Hero’ wimbo huo ulimtambulisha katika tasnia ya Bongo Fleva kama mwanamuziki ambapo mpaka sasa imetazamwa zaidi ya mara  milioni mbili kwenye YouTube. Lakini mwaka huo alitoa wimbo ‘Tunaendana’.

Mwaka 2021, alizindua lebo yake ya Muziki inayofahamika kama Mobetto Music na mwaka huo huo alifanikiwa kutoa remix ya wimbo wa Ex wangu ngoma ya kwake Seneta Kilaka na kuweza kutengeneza video kali iliyotazamwa zaidi ya mara milion 11 YouTube.

Mwaka 2022 alitoa Ep yake ya ‘Your Truly’ iliyokuwa na nyimbo sita, ambazo ni Wazamani, Pop it, Wewe Ft Otile Brown, Murua na Want.