Hamdi apitisha panga Yanga wanne hatarini

Mikakati ya kukiimarisha kikosi cha Yanga kwa ajili ya msimu ujao, imeanza mapema kwa kocha wa timu hiyo, Hamdi Miloud kuwasilisha ripoti ya usajili ambayo ameainisha nyota wanne anaowataka.

Yanga ambayo Jumatatu hii itakuwa Manyara kucheza na Fountain Gate mechi ya Ligi Kuu Bara, inapambana kubeba ubingwa wa michuano hiyo kwa msimu wa nne mfululizo.

Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 67 baada ya kucheza mechi 25, zikibaki tano kumaliza msimu.

Sasa katika hesabu za msimu ujao, Hamdi amepeleka ripoti ya usajili kwa mabosi wa klabu hiyo, akitaka wamshushie mshambuliaji, beki wa kati, kiungo mkabaji na namba kumi ya maana.

Taarifa ilizonazo Mwanaspoti ni kwamba kocha ametaka yafanyike maboresho ya kikosi katika baadhi ya maeneo ambayo yatakwenda kuongezea nguvu ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao.

“Kocha ametaka mastaa wenye uwezo mkubwa waongezwe katika maeneo makubwa manne kwa ajili ya msimu ujao ili kuongeza nguvu kwenye mashindano yote timu itakayoshiriki.

“Ripoti hiyo inataka mshambuliaji wa mwisho, namba kumi mwingine bora, beki wa kati na kiungo mkabaji, ingawa waliopo wanafanya kazi nzuri lakini kikosi kinatakiwa kuwa kizito zaidi ili kufanya vizuri kuanzia michuano ya ndani hadi kimataifa,” kilisema chanzo.

HALI ILIVYO

Katika maeneo hayo ambayo Hamdi ameyataja yaongezewe nguvu, kwa sasa yana watu wa maana, lakini bado kocha huyo anahitaji nguvu ya ziada.

Yanga ina viungo wakabaji watano ambao kati yao wawili mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu, ambao ni Jonas Mkude aliyekosa nafasi ya kucheza na Khalid Aucho anayesumbuliwa na majeraha.

Duke Abuya na Mudathir Yahya, ndiyo wanacheza kwa sasa, huku Salum Abubakar ‘Sure Boy’ naye hana nafasi kubwa.

Upande wa ushambuliaji, wapo Clement Mzize mwenye mabao 10 katika Ligi Kuu na Prince Dube aliyefunga 12. Pia Kennedy Musonda (3) ambaye mkataba wake unaisha msimu huu.

Wakati Musonda mkataba ukienda kumalizika, Mzize ana ofa kadhaa kutoka timu mbalimbali nje ya Tanzania, hivyo kuna uwezekano akaondoka.

Kikosi hicho katika beki wa kati kuna Dickson Job na Ibrahim Bacca wenye nafasi kubwa ya kucheza huku nahodha Bakari Mwamnyeto akiwasubiri benchini.

Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI na Clatous Chama ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni, ndiyo wanaocheza eneo la namba kumi. Aziz Ki naye anatajwa kuwa njiani kuondoka.

Hivyo inahitaji mashine mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *