Hamdi aja na mkakati wa siku 5 Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi amesema licha ya ugumu wa ratiba iliyonayo timu hiyo, lakini ametengeneza mkakati kabambe wa siku tano ili kuendelea kugawa dozi kama kawaida katika Ligi Kuu kabla ya kuhamishia makali visiwani Zanzibar katika mechi za michuano ya Kombe la Muungano 2025.

Yanga inatarajia kusafiri hadi Manyara kukabiliana na Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu itakayiopigwa Jumatatu kabla ya kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Muungano ikipangwa kuanza na KVZ Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja.

Kocha Hamdi, alisema wanasafiri kuifuata Fountain Gate wakiwa na siku tatu tu kabla ya kwenda Zanzibar kwa michuano ya Muungano na kwamba sio ratiba rahisi, lakini anajivunia ubora wa wachezaji alionao hasa wasiopata nafasi ya kucheza ambao amepanga kuwatumia kwa mechi hizo za visiwani.

“Kiukweli tuna ratiba ngumu kidogo, lakini tunapangilia ili kutoa angalau nafasi kwa wachezaji wengine kucheza michuano iliyo mbele yetu. Hatupaswi kulalamika isipokuwa kupambana na hali halisi, ingawa ukweli ni kwamba najivunia kikosi nilichonacho naamini hakitaniangusha.”

Aidha, kocha Hamdi alisifu upana na utajiri wa kikosi chake kuwa unampa nafasi kubwa kutumia mfumo wowote bila kuathiri ufanisi wa timu.

“Kama ulifuatilia mchezo uliopita dhidi ya Stand United kulikuwa na mabadililo na nilitoa nafasi kwa wachezaji wengi ambao hawana uhakika wa kucheza mara kwa mara na wameonyesha kwa kufanya vizuri imenipa picha nzuri ya kuendana na ratiba iliyo mbele yetu,”

“Kila mashindano yaliyo mbele ni muhimu kwetu hivyop tutatumia wachezaji kulingana na mahitaji kuhusu mchezo wa Jumatatu tunahitaji matokeo ni mchezo muhimu kujihakikishia nafasi ya kutetea taji na kuendelea kuwaacha mbali zaidi wapinzani wetu.”

Alisema Yanga wana utajiri mkubwa wa vipaji ambao unampa wasaa wa kutumia mfumo wowote bila kuathiri ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja. Ingawa yeye sio muumini wa mfumo  bali anaangalia namna gani sahihi ya kutengeneza nafasi na kuzitumia.

Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa siku ya Jumatatu dhidi ya Fountain Gate ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Desemba 29 mwaka jana, huku ikipuiga hesabu ya kutetea taji inalolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *