Hamdi agawa dakika 270

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, ameonekana kuridhishwa na safu yake ya ulinzi huku akizigawa dakika 270 zilizoleta matumaini makubwa.

Hamdi ambaye ameiongoza Yanga katika mechi sita za Ligi Kuu Bara, ana jukumu kubwa la kuhakikisha timu hiyo inatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliouchukua misimu mitatu mfululizo.

Katika mechi tatu za kwanza ambazo ni dakika 270 dhidi ya JKT Tanzania (0-0), KMC (6-1) na Singida Black Stars (2-1), Yanga iliruhusu mabao mawili, lakini tatu zilizofuatia ikaondoka na clean sheet ambazo ni dhidi ya Mashujaa (5-0), Pamba Jiji (3-0) na Tabora United (3-0).

Katika mbio za kufikia malengo ya kutetea ubingwa, hadi sasa Hamdi amekoshwa na namna safu yake ya ulinzi inavyofanya kazi kubwa ya kutoruhusu mabao kirahisi tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Yanga ikiwa imecheza mechi 23 za ligi msimu huu, imeruhusu mabao tisa, kati ya hayo mawili yamepatikana chini ya Hamdi.

Akizungumzia uimara wa safu yake ya ulinzi, Hamdi ameliambia Mwanaspoti kuwa wakati anakabidhiwa kikosi alikuta changamoto ya eneo lake la ulinzi kutokuwa na utulivu.

Hamdi amesema hali hiyo iliwafanya kuruhusu mabao mawili yaliyoonekana ni rahisi katika mechi zake tatu za kwanza lakini baada ya kuifanyia maboresho imempa matumaini makubwa kutokana na kucheza mechi tatu mfululizo bila ya nyavu zao kutikiswa.

“Shida kubwa ilikuwa kwenye utulivu wa mabeki wangu, lakini pia uimara wa eneo la katikati ambapo kwa sasa yameanza kuwa na mabadiliko.

“Natamani sana ubora huo uendelee zaidi, kwani tumebakiza mechi chache ambazo hatutakiwi kupoteza ili kuchukua ubingwa msimu huu.

“Malengo ya timu ni kuwa washindi tena, hivyo naamini katika ubora wa mastaa wangu wote na kwa pamoja tunaweza kufanikisha hayo yote,” alisema Hamdi.

Msimu huu Yanga imefundishwa na makocha watatu, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na sasa Hamdi Miloud.

Gamondi aliiongoza Yanga katika mechi kumi ambapo nane za kwanza alicheza bila ya kuruhusu bao, kabla ya nyavu zao kutikiswa mara nne katika mechi mbili dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1). Safari yake ikaishia hapo.

Ramovic akawa kocha wa pili ambapo aliiongoza katika mechi sita akiruhusu mabao mawili. Matokeo ya mechi zake ni dhidi ya Namungo (2-0), Mashujaa (3-2), Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), Fountain Gate (5-0) na Kagera Sugar (4-0).

Baada ya hapo ndipo kocha Hamdi alitambulishwa kuwa kocha wa Yanga, huku katika mchezo wake wa kwanza alikuwa jukwaani akiishuhudia timu hiyo ikishinda 6-1 dhidi ya KenGold, benchi likiongozwa na Abdihamid Moallin.

Mechi zilizofuatia Yanga ilitoka 0-0 na JKT Tanzania, kisha ikashinda zote dhidi ya KMC (6-1), Singida Black Stars (2-1), Mashujaa (5-0), Pamba Jiji (3-0) na Tabora United (3-0).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *