
YANGA walikuwa bize kuijadili sare iliyopata Simba dhidi ya Fountain Gate na kusahau kama walikuwa na mechi ngumu dhidi ya maafande wa JKT Tanzania na kujikuta leo nao wakipoteza pointi mbili kwa kupata sare ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mashabiki wa Yanga sambamba na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo waliungana kuijadili sare hiyo ya Simba iliyopata ugenini, huku wakimkejeli Ladack Chasambi aliyejifunga bao katika mechi hiyo, lakini wakasahau kama nao walikuwa na mechi ya ugenini dhidi ya JKT na kujikuta wakidondosha pointi.
Matokeo hayo ya leo yameiweka rehani Yanga kuendelea kusalia kileleni, kwani Simba jioni ya Jumanne hii inashuka uwanjani kucheza dhidi ya Tanzania Prisons na iwapo itashinda itakuwa na nafasi ya kuing’oa na kurejea pale patamu kwa kutofautiana kwa pointi moja kwani itafikisha 47, wakati Yanga ina 46 baada ya michezo mechi 18.
Hiyo ni sare ya pili kwa Yanga mbele ya JKT kwenye uwanja huo, kwani msimu uliopita pia ilitoka suluhu na kumfanya kocha mpya wa timu hiyo, Miloud Hamdi kuanza kazi Jangwani kwa kuambulia pointi moja.
NIDHAMU KIWANGO CHA SGR
Katika mchezo wa leo makocha Ahmad Ally wa JKT na Hamdi wa Yanga walionekana kuzipanga vyema timu zao, Wananchi wakianza kwa kupoteza nafasi nyingi, shukrani kwa ‘sevu’ za kibabe za kipa, Yakubu Suleiman, na uchezaji wa nidhamu ya kiwango cha SGR wa kikosi kizima cha wanajeshi wa JKT kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.
Haikushangaza mwisho wa mchezo, beki wa kati Wilson Nangu, aliposhinda tuzo ya Nyota wa Mchezo, baada ya kuwa kizingiti cha kuwafanya mastraika wa Yanga wasifurukute, akionyesha kuwa hii ligi anaimudu licha ya kuwa ndio msimu wake wa kwanza kucheza michuano hiyo akitokea katika timu ya TMA ya Ligi ya Championship.
Kocha mpya wa Yanga, Hamdi ambaye alikaa kwa mara ya kwanza kwenye benchi la timu hiyo ya Jangwani kuiongoza timu hiyo katika mechi ya ligi tangu alipotambulishwa Februari 4, 2025, alishuhudia mbinu zake zikishindwa kuzaa matunda tarajiwa.
Juhudi za washambuliaji wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize kulishambulia lango la JKT Tanzania, zilizimwa na walinzi wa kati, Nangu aliyekuwa akishirikiana vema na nahodha Edson Katanga huku kipa Yakubu akiwa imara langoni.
Eneo la kiungo cha kati la JKT Tanzania lilionekana kuyumba hasa kwenye ukabaji hali iliyomlazimu kocha Ahmad Ally wakati kipindi cha pili kikitaka kuanza alimtoa Ally Msengi na kuingia Edward Maka, huku pia akiimarisha ulinzi wa kulia akimtoa George Wawa nafasi yake akachukua Salum Khamis Salum.
Kabla ya mabadiliko hayo, JKT Tanzania ilionyesha ukomavu wa kushambulia na kuzuia huku kipa Yakubu Suleiman akiokoa nafasi ya wazi ambayo Mzize ilibaki kidogo afunge katika dakika ya 45 na kuwa kona ya kwanza ya mchezo huo.
JKT Tanzania wamekuwa wagumu wanapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani kwani hawajapoteza mchezo msimu huu wakishinda mechi tatu na sare tano, wakifunga mabao saba na kuruhusu matatu, wakiondoka na ‘clean sheet’ sita.
Yanga ambayo ilikuwa inapambania pointi tatu za kuifanya ikae kileleni kwa amani, ilikuwa inaifukuzia rekodi yake ya kushinda mechi zote za ugenini kwenye ligi msimu huu baada ya kucheza saba kabla ya kukutana na JKT Tanzania ikifunga mabao 12 na haijaruhusu bao, clean sheet zikiwa saba, lakini jana ikaongeza clean sheet ya nane, ila rekodi ya kushinda mfululizo ikafikia ukomo.
Katika kukutana kwao tangu msimu wa 2018-2019, Yanga imeshinda 7 na kufunga mabao 18, sare zikiwa 3, wakati JKT haijashinda ikifunga mabao 3.
Mara ya mwisho timu hizi kucheza uwanjani hapa ilikuwa Aprili 24, 2024 na matokeo yakawa suluhu 0-0. Na sasa katika mechi sita za mwisho JKT haijafunga bao dhidi ya Yanga, mara ya mwisho ilifunga bao Juni 17, 2020 katika sare ya 1-1
SHUGHULI ILIKUWA PEVU
Mchezo ulitawaliwa na matukio mengi ya kuchezeana kwa nguvu lakini ilishuhudiwa kipindi cha kwanza licha ya kufanyika jumla ya faulo 20, lakini mwamuzi Ahmed Arajiga hakuonyesha kadi yoyote.
Miongoni mwa matukio ya kushangaza ni namna walinzi wa JKT Tanzania walivyokuwa wakomkaba Dube na kumsababishia kubadili jezi mapema dakika ya nane baada ya ile ya kwanza kuchanika.
Kipindi cha pili, mwamuzi Arajiga alikuwa mkali kwani dakika 25 za kwanza aliwaonyesha kadi za njano wachezaji wanne, Salum Khamis Salum, Hassan Maulid Nassoro na Wilson Nangu wa JKT Tanzania sambamba na Kennedy Musonda wa Yanga.
Staa wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ambaye kuelekea mechi hii leo alitingisha nchi baada ya kuzagaa kwa taarifa kwamba anajiandaa kumuoa mwanamitindo Hamisa Mobetto, alianzia benchini dhidi ya JKT na akaingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Clatous Chama, lakini hakuweza kusaidia kubadilisha matokeo ya suluhu hiyo.
JKT TZ: Yacoub Suleiman, George Wawa/Salum Khamis, Karimu Mfaume, Edson Katanga, Wilson Nangu, Ally Msengi/Maka Edward, Najim Maguru, Hassan Maulid, Gamba Matiko, Hassan Dilunga/Ismail Aziz na Jafary Maneno/Said Ndemla.
YANGA: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Hamad, Khalid Aucho, Clement Mzize/Kennedy Musonda, Mudathir Yahya/Duke Abuya, Prince Dube, Clatous Chama/Aziz Ki na Pacome Zouzoua/Maxi Nzengeli.
KMC YAIZIMA SINGIDA
Katika mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge Dar es Salaam wenyeji KMC waliiwaduwaza Singida Black Stars kwa kuifumua mabao 2-0 yote yakiwekwa kimiani na Oscar Paul katika kipindi cha kwanza.
Mfungaji huyo alianza kwa kufunga katika dakika ya 35 akiwahi mpira ulioshindwa kuokolewa vyema na mabeki wa Singida na kufumua shuti lililomshinda kipa Hussein Masalanga kabla ya kuongeza jingine dakika tano baadye kwa kumalizia pasi ya Daruwesh Saliboko.
Matokeo hayo yameifanya KIMC kufikisha pointi 22 na kuchupa kutoka nafasi ya 11 hadi ya sita, huku Singida ikisalia nafasi ya nne ikiwa na pointi 33 na ikiwa haijaonja ushindi katika mechi tatu zilizopita baada ya kulala 1-0 mbele ya Simba, kisha kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar mechi iliyopita.