Afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amethibitisha kuwa kiongozi wa harakati hiyo, Yahya Sinwar, ameuawa shahidi katika shambulizi la anga la Israel katika mji wa Rafah huko Gaza.
Khalil al Hayya, mkuu wa Hamas huko Gaza, ametoa taarifa huyo leo Ijumaa, siku moja baada ya ripoti za kuuawa shahidi Yahya Sinwar.
Al Hayya amemtaja Yahya Sinwar kuwa alikuwa “imara, shujaa na jasiri” na kwamba alisabilia maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa watu wa Palestina.
“Sinwar ameishi maisha yake yote kama mpiganaji wa Jihadi. Tangu siku za awali za maisha yake, alikuwa akijishughulisha na mapambano kama mwanamuqawama”, amesisitiza Khalil al Hayya.
Kiongozi huyo wa Hamas alinusurika majaribio mengi ya mauaji kabla na baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023.
Sinwar, aliyekuwa na umri wa miaka 62, alikuwa na nafasi kubwa katika kuratibu na kusimamia operesheni hiyo ya kihistoria iliyoutikisa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kabla ya kuwa kiongozi wa Hamas huko Gaza mnamo 2017, Sinwar alifungwa miaka 22 katika jela ya Israel. Aliachiliwa huru kama sehemu ya ubadilishaji wa wafungwa mnamo 2011.
“Hamas kamwe haitaacha njia ya Muqawama… mapambano yetu ya yataendelea hadi Palestina yote itakapokombolewa,” alisema Yahya Sinwar wakati wa hotuba yake huko Gaza mwishoni mwa Oktoba 2017.