Hamas yasema, harakati hiyo haiwezi kuanganizwa kwa ‘kuuawa viongozi wake’

Afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema harakati hiyo inayopigania ukombozi wa Palestina kutoka kwenye makucha ya utawala ghasibu wa Israel haiwezi kuangamizwa kwa “kuuawa viongozi wake”.

Basem Naim, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, ameyasema hayo leo Ijumaa, siku moja baada ya Israel kudai kuwa imemuua kiongozi wa harakati hiyo katika Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar.

“Hamas ni harakati ya ukombozi inayoongozwa na watu wanaopigania uhuru na utu, na haiwezi kumalizwa,” amesema Basem Naim katika taarifa yake na kuongeza kuwa: “Tunaamini kwamba, hatima yetu ni moja ya mambo mawili mazuri, ama ushindi au kuuawa shahidi.”

Naim amesema: “Ndiyo inatia uchungu na inahuzunisha sana kupoteza watu tunaowapenda, hasa viongozi wa aina yake kama wetu sisi, lakini tuna uhakika kwamba haya ndiyo matokeo ya watu wote waliopigania uhuru wao.”

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, jeshi la Israel lilidai kuwa Sinwar “ameuawa” na wanajeshi wa utawala huo kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Yahya Sinwar

Israel ilianzisha mashambulizi ya mauaji ya kimbari huko Gaza baada ya Hamas kutekeleza Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana kulipiza kisasi kwa ukatili uliokithiri wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.