Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imelaani mashambulizi makali yaliyofanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel dhidi ya jengo la makazi ya raia na kuua makumi ya watu katika Ukanda wa Gaza. Taarifa iliyotolewa na Hamas imesisitiza kwamba vitendo hivyo vya kichokozi havitavunja irada na azma thabiti ya watu wa Palestina.
Makumi ya Wapalestina waliuawa mapema jana Jumapili katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya jengo la ghorofa tano katika eneo la Beit Lahiya huko kaskazini mwa Gaza, huku wengine wakiwa wamekwama chini ya vifusi.
Idara ya Masuala ya Dharura ya Kiraia ya Palestina imesema karibu watu 70 walikuwa wakiishi katika jengo hiyo.
Taarifa ya Hamas imesema: “Shambulio la kijinai lililofanywa na jeshi la kifashisti ambalo limelenga jengo la makazi ya raia huko Beit Lahiya, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na kuliharibu juu ya vichwa vya wakazi wake – na kusababisha mauaji ya zaidi ya raia hamsini, zaidi ya theluthi moja wakiwa watoto- ni kitendo cha wazi cha mauaji ya kimbari ya Wazayuni, mauaji ya halaiki, na kuua raia wasio na ulinzi.”

Hamas imesisitiza kwamba umwagaji damu huo ni mwendelezo wa mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasio na ulinzi, na kuongeza kuwa: “Ukatili huu unafanyika mbele ya masikio na macho ya ulimwengu.”
Hamas imesisitiza kwamba kuendelea kwa mauaji hayo ya kimbari na kampeni za kuwatesa watu kwa njaa vinavyolenga “kuwafukuza watu wetu na kuangamiza mapambano ya ukombozi wa taifa hakutafikia malengo yake au kuvunja azma ya watu wetu.”
Hamas pia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, na nchi za Kiarabu na Kiislamu kuvunja kimya chao kuhusiana na uhalifu huu na kuchukua hatua za haraka za kukomesha mauaji yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza, hasa kaskazini mwa eneo hilo.