HAMAS yalaani kimya cha walimwengu baada ya Israel kuvamia hospitali na kuua watoto ndani yake

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema jumuiya na taasisi za kimataifa zinabeba dhima ya kisiasa na kimaadili kwa jinai zinazoendelea kufanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Hamas imeeleza hayo katika taarifa iliyotoa jana Ijumaa na kusisitiza kwamba Jamii ya Kimataifa inabeba dhima hiyo kutokana na kimya inachoonyesha mbele ya uhalifu huo.

Taarifa ya Harakati hiyo ya Muqawama wa Palestina imeongeza kuwa, kimya hicho kimepelekea “kuporomoka kwa mfumo wa maadili na sheria za kimataifa kutokana na ukiukaji mkubwa wa sheria unaofanywa na Wazayuni”.

Matamshi hayo yametolewa baada ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel kuvamia hospitali ya Kamal Adwan katika mji wa Beit Lahia, ambayo ni hospitali ya mwisho inayofanya kazi karibu na eneo la Jabalia lililozingirwa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Katika uvamizi huo Jeshi la utawala wa Kizayuni liliripua “kituo cha oksijeni” katika hospitali hiyo, na kuua watoto kadhaa.

Hamas imesema, ukatili huo “ni uhalifu wa kivita na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa”.

Mbali na jinai hiyo askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni waliwakamata waliokuwemo hospitalini humo, ambapo makumi ya waliokamatwa walilazimishwa kuvua nguo zao kabla ya kukusanywa katika eneo la wazi nje ya hospitali hiyo.

Hayo yameripotiwa na Wakala wa Habari wa Palestina wa Mtandao wa Habari wa Quds, na kuongeza kuwa hatima ya waliokamatwa haijulikani.

Idhilali waliyofanyiwa Wapalestina waliokuwemo Hospitalini na askari wa Kizayuni

Hamas ilisema uvamizi dhidi ya Hospitali ya Kamal Adwan umefanywa “saa chache baada ya kuiwekea mzingiro” hospitali hiyo, kitendo ambacho kilifuatiwa na kukamatwa na kunyanyaswa wagonjwa, majeruhi, wafanyikazi wa kada ya tiba, familia zilizohamishwa, na wanaharakati wa vyombo vya habari, ambao walipelekwa mahali kusikojulikana.

Harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imeendelea kubainisha katika taarifa yake kwamba, utawala dhalimu wa Kizayuni unaendeleza mauaji ya kimbari kaskazini mwa Ghaza, bila kujali matokeo yake, huku ukisaidiwa na kuungwa mkono kikamilifu na utawala wa Marekani.

Hamas imemalizia taarifa yake yake kwa kutoa wito kwa nchi za Kiislamu, yakiwemo mataifa ya Kiarabu kuwajibika kwa kwenda mbali zaidi ya kutosheka na kutoa kauli tupu za kulaani, kwa kuchukua hatua ili kukomesha mauaji ya kimbari na maangamizi ya kizazi ambayo yamekuwa yakifanywa dhidi ya Wapalestina…/