Hamas yaikabidhi Israel mabaki halisi ya Shiri Bibas, familia yathibitisha

Tel Aviv. Familia ya Bibas kutoka Israeli imethibitisha kuwa mabaki ya Shiri Bibas yamerejeshwa na Hamas, siku moja baada ya kudai kuwa kundi hilo lilikuwa limekabidhi mwili ambao siyo wa mpendwa wao.

Jana, Ijumaa, Hamas ilikabidhi mabaki ya Bibas baada ya utambulisho wa awali uliofanyika vibaya na kusababisha hasira miongoni mwa raia na viongozi wa Serikali nchini Israeli, hali ambayo ilihatarisha makubaliano kusitisha mapigano huko Gaza.

Ukoo wa Bibas wenye makazi yake eneo la Kibbutz Nir Oz nchini Israel ulithibitisha utambulisho wake Jumamosi, saa chache kabla ya ubadilishanaji wa mateka dhidi ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.

“Baada ya mchakato wa utambuzi katika Taasisi ya Tiba ya Uchunguzi wa vifo, asubuhi ya leo tumepokea habari nzuri na ya kushtua. Shiri wetu aliuawa akiwa mateka na sasa amerudi nyumbani kwa wanawe, mumewe, dada yake na familia yake yote ili apumzike,” familia ya Bibas ilisema katika taarifa iliyochapishwa Jumamosi.

Hamas ilikubali kukabidhi miili ya Bibas na wanawe wawili wadogo, Kfir na Ariel, pamoja na mabaki ya mateka wa nne Alhamisi iliyopita, chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yamesitisha mapigano huko Gaza tangu Januari 19, 2025.

Hamas ilisema watoto hao na mama yao waliuawa katika shambulio la anga la Israeli Novemba 2023. Hata hivyo, Israel imekanusha madai hayo na kusema raia hao waliuawa na wapiganaji wa Hamas.

Miili minne ilikabidhiwa, lakini baadaye Israeli ilisema kuwa moja ya mabaki hayo hayakuwa ya Shiri Bibas.

Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliahidi kuhakikisha Hamas inalipa gharama kwa kile alichoeleza ni uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Baadaye Hamas ilikiri kufanyika makosa ama mkanganyiko wa miili hiyo na kueleza kuwa hali hiyo ilisababishwa na mabomu ya Israeli katika eneo hilo ambayo yaliwaua watu kadhaa.

Basem Naim ambaye ni mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, amesema makosa yasiyotarajiwa yanaweza kutokea, kwa kile alichodai mabomu ya Israeli yaliwachanganya mateka wa Israeli na Wapalestina, ambapo maelfu bado wamefukiwa chini ya vifusi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israeli.

“Tunathibitisha kuwa siyo sehemu ya maadili yetu au maslahi yetu kuweka miili yoyote au kutotii makubaliano tunayotia saini,” alisema katika taarifa yake.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza inayoongozwa na Hamas, Ismail al-Thawabta, alisema Netanyahu ndiyo anayepaswa kuwajibishwa kwa vifo vya Shiri na watoto wake.

Tukio hili limeonyesha udhaifu wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kwa msaada wa Marekani na wapatanishi wa Qatar na Misri mwezi uliopita.

Watu sita walioko hai wanatarajiwa kuachiliwa huru leo Jumamosi kwa kubadilishana na Wapalestina 602 walioko gerezani Israeli, wengi wao wakiwa wamekamatwa bila kushtakiwa. Mazungumzo ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano yanatarajiwa kuanza katika siku zijazo.

Imeandikwa na Mgongo Kaiitira kwa msaasa wa Mashirika.