HAMAS yaendelea kuangamiza wanajeshi wa Israel kaskazini mwa Ghaza

Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS zimetangaza kuwa zimeangamiza maafisa wengine watatu wa jeshi la utawala wa Kizayuni na zana zao za kijeshi kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Taarifa ya HAMAS imesema kuwa, jana Ijumaa harakati hiyo iliteketeza zana za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la Bait Lahya la kaskazini mwa Ukanda wa Gahza na kuangamiza pia maafisa wa kijeshi wa Israel.

Katika ushahidi wa picha na video uliooneshwa na tawi hilo la kijeshi la HAMAS kunaokena kifaru cha Merkava cha Israel katika eneo la Tel al Dhahab kikipigwa kwa roketi la Yasin 105 na pia buldoza moja la D9 na kifaru kingine cha Israel kikiteketezwa kwa maroketi ya Yasin 105 katika eneo la al Shaima kaskazini mwa Ghaza. 

Taarifa hiyo ya HAMAS imeongeza kuwa, wanamapambano wa harakati hiyo wameangamiza pia maafisa watatu wa kijeshi wa Israel karibu na medani ya Abbas Kilani, kaskazini mwa mji wa Bait Lahya, kaskazini mwa Ghaza. 

Pia wanamapambano hao wa HAMAS wameteketeza kivaru kingine cha Merkava 4 cha jeshi la Israel katika barabara ya Daous magharibi mwa kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kaskazini mwa Ghaza.