Hamas yaahirisha kuachiliwa tena kwa mateka, Israel yalaani ‘ukiukaji kamili’ wa usitishjia vita

Hamas imetangaza Jumatatu, Februari 10, “hadi hatua nyingine takapochukuliwa” kuachiliwa tena kwa mateka wa Israel waliotekwa huko Gaza,zoezi ambalo kawaida lilikuwa limepangwa kufayka siku ya Jumamosi, Februari 15. Israel inachukulia hili kama “ukiukaji kamili” wa makubaliano ya kusitisha mapigano na inatayarisha jeshi lake “kwa hali zote.” Saa chache baadaye, Hamas ilifafanua kwamba “mlango unabaki kuwa wazi kwa mabadilishano ya wafungwa yanayofuata kufanyika kulingana na mpango uliopangwa.”

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Makubaliano ya usitishaji mapigano yanayoendelea kati ya Israeli na Hamas, kuanzia Januari 19, yako hatarini kufuatia misimamo iliyochukuliwa na kambi hizo mbili siku ya  Jumatatu, Februari 10. Tawi lenye silaha la Hamas limetangaza kwa mara ya kwanza kwamba linaahirisha “hadi hatua nyingine itakapochukuliwa” kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza.

“Kuachiliwa kwa wafungwa hao, kulikopangwa Jumamosi ijayo, Februari 15, 2025, kumeahirishwa hadi hatua nyingine itakapotangazwa ili kusubiri wavamizi (Israel) kutekeleza majukumu yake,” amesema Abu Obeida, msemaji wa Brigedi ya Ezzedine al-Qassam, katika taarifa yake. Mateka watatu wanatarajiwa kuachiliwa mnamo Februari 15.

Majibu ya Waisraeli yalikuwa ya haraka. Kikao cha baraza la mawaziri la usalama la Israel mjini Jerusalem kimesogezwa mbele hadi saa 11 alfajiri ya leo Jumanne kwa saa za Israeli. Waziri wa Ulinzi Israel Katz pia alisema katika taarifa yake kwamba “tangazo la Hamas la kusitisha kuachiliwa kwa mateka wa Israel ni ukiukaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka.” Matokeo yake, jeshi la Israeli liliamriwa “kujiandaa kwa matukio yote.” Vikosi vya jeshi la Israeli vimetangaza jioni kwamba “wanaimarisha kwa nguvu eneo (karibu na Ukanda wa Gaza) kwa askari wa ziada kwa ajili ya misheni za ulinzi.”

Kwa mujibu wa Israeli, mgogoro huo unahusu hasa utekelezaji wa itifaki ya kibinadamu ya makubaliano. Hasa zaidi, juu ya kuingia kwa misafara 60,000 katika Ukanda wa Gaza. Mzozo, imebainishwa hapa, ambao unaweza kutatuliwa.

Mrengo wa kulia wa Israeli, ambao unaunga mkono kuanzishwa tena kwa vita, unachukua fursa hii kusisitiza maoni yake tena, anaripoti Michel Paul huko Jerusalem. Waziri wa zamani Itamar Ben Gvir anatoa wito wa shambulio kubwa Gaza, kwa wasiwasi mkubwa wa familia za mateka, ambao wanaomba wapatanishi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo. “Kila dakika ni muhimu kwa mateka ambao bado wanashikiliwa huko Gaza,” Jukwaa la Familia linasisitiza.

Saa chache baada ya taarifa yake ya kwanza na majibu ya Israel, Hamas imechapisha taarifa mpya ambapo ilihakikisha kwamba mabadilishano mapya yanawezekana kulingana na mpango uliowekwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano. “Mlango unabaki wazi kwa mabadilishano yajayo ya wafungwa kufanyika kulingana na mpango uliopangwa, mara [Israeli] itakapokuwa imetimiza wajibu wake,” limesema vuguvugu hilo, ambalo linadai kuwa “kwa makusudi” limetangaza kuahirishwa kwa muda usiojulikana wa kuachiliwa kwa mateka “ili kuwapa wapatanishi muda wa kutosha kuweka shinikizo kwa Israeli.”