HAMAS: Andamaneni na zidini kuzizingira balozi za utawala wa Kizayuni na wanaouunga mkono

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa wito wa kuzidishwa harakati za umma katika ngazi ya kimataifa katika kulaani mwendelezo wa jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kuliunga mkono taifa la Muqawama la Palestina.

Hamas ilitoa mwito huo jana Jumatano kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na watetezi wa ukombozi na uhuru duniani kote kukithirisha zaidi harakati zao, maandamano na matembezi yao siku ya Ijumaa na Jumamosi katika miji mikuu na miji mingine yote ya nchi za Kiarabu, za Kiislamu na nchi zingine duniani, kwa kuzingira balozi za utawala wa Kizayuni na za nchi zinazouunga mkono utawala huo dhalimu.

Katika wito wake huo, Hamas imewataka walimwengu walaani zaidi kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, kuzingirwa kikamilifu eneo la kaskazini la ukanda huo, na kukazania utawala huo ghasibu kuendeleza vita vya mauaji ya kimbari na kuwatesa kwa njaa raia Wapalestina wasio na ulinzi katika eneo hilo; na vilevile kuanika hadharani na kulaani uungaji mkono wa Marekani, Uingereza na Ujerumani kwa wavamizi wa Kizayuni katika vita na uchokozi wao dhidi ya Ghaza.

Kadhalika, Harakati ya Hamas imebainisha kuwa, jicho la matumaini ya wananchi wanamuqawama wa Palestina huko Ghaza limeelekezwa kwa Umma wa Kiislamu na Kiarabu na watetezi wa uhuru duniani, ili kwa kushiriki kwao kikamilifu katika maandamano hayo watumie kila wenzo kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel na waungaji mkono wake wakomeshe uchokozi dhidi ya Ghaza na kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina…/