
Unguja. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amechukua fomu kuwania urais Zanzibar, akieleza vipaumbele vyake ni kujikita kwenye kilimo, elimu, afya, mazingira na utalii.
Amechukua fomu hiyo leo Mei 18, 2025 katika ofisi za chama hicho Mtopepo Mjini Unguja huku akieleza nia yake ya kutoa fursa kwa wakulima na kuisaidia Zanzibar kuondoa daraja lililopo la kipato miongoni mwa wananchi.
Hamad anakuwa mtu wa tatu kuonyesha nia kuwania urais wa Zanzibar.
Hamad Rashid anakwenda kuchuana na Rais Hussein Mwinyi ambaye tayari ameshapitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania muhula wa pili.
Mwinyi pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan waliteuliwa na Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18 na 19, 2025 Mjini Dodoma kupeperusha bendera ya chama hicho.
Mwingine aliyechukua fomu kuwania nafsi hiyo kwa Zanzibar ni Othman Masoud ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alichukua fomu Aprili 12, 2025 na kurejesha Aprili 16, 2025 katika ofisi kuu za chama hicho, Vuga, Zanzibar.
Akizungumza leo Mei 18, 2025 baada ya kuchukua fomu, Hamad Rashid amesema anaomba nafasi hiyo kwa dhati ili kuisaidia Zanzibar katika mambo mengi.
“Nataka kwanza kuunganisha wananchi, kati ya wenye nacho na wasio nacho ili kwa pamoja kuleta usawa wa kimaendeleo,” amesema Hamad.
Amesema iwapo akishika nafasi hiyo, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kwenye kilimo kuwapatia fursa wakulima wazalishe kwa wingi.
Amesema hali ya upatikanaji wa chakula kwa Zanzibar hairidhishi akitaja sababu kubwa ni kukosekana msukumo wa dhati kuinua sekta ya kilimo.
“Wakulima ndio wazalishaji wakubwa lakini bado kilimo chetu hakijaleta tija na hilo ndio pengo kubwa linalosababisha watu wa hali ya chini wasiinuke, kwani wengi wanategemea kilimo,” amedai.
Amedai bei ya vyakula nayo hairidhishi hivyo kuongeza umasikini.
“Kwa hiyo nimechukua fomu kuomba ridhaa iwapo chama changu kikinipitisha tunaenda kushughulikia changamoto hizi,” amesema.
Katika upande wa elimu ataipa nafsi elimu ya teknolojia, sayansi na ufundi kuanzia chekechea, madrasa hadi vyuo vikuu na vya ufundi kwa kutayarisha walimu wa masomo hayo.
Vilevile, kipaumbele chake kingine ni kuwa na taasisi za afya za kufanya utafiti wa maradhi mbalimbali ikiwemo saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Amesema atahakikisha kunakuwa na hospitali za kitaifa za rufaa moja Unguja na nyingine Pemba ambazo zitasaidia kupunguza wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi.
Kwa upande wa makazi, Hamad amesema atajenga majumba ya ghorofa nchi nzima kwa kutumia teknolojia isiyotumia rasilimali za mchanga wa ndani ya nchi, na kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kukahakikisha utunzaji wa majabali, fukwe na miti.
Amesema licha kuwa na vivutio vingi, Zanzibar bado haijatumia kikamilifu fursa za utalii wa kiutamaduni, kiikolojia na kihistoria na uwekezaji mdogo katika miundombinu ya utalii na uendelezaji wa vivutio vya ndani.
Hivyo, anatarajia kuimarisha utalii wa kiutamaduni na kihistoria, kukuza utalii wa urithi kwa kuboresha maeneo ya kihistoria kama Mji Mkongwe na ngome za kale.
“Tutaanzisha maonyesho ya utamaduni wa Zanzibar ili kuwavutia wageni wengi kuja kuwekea,” amesema.