
UNAMKUMBUKA beki wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyewahi kuwika na Mtibwa Sugar kabla ya kwenda Kenya kujiunga na Sofapaka na kisha AFC Leopards, Idrisa Rajabu?
Beki huyo wa pembeni aliyekuwa sehemu ya kikosi cha Mtibwa kilichobeba Kombe la Tusker 2008 na mmoja ya wachezaji waliokuwa tegemeo wa timu ya taifa, Taifa Stars kwa sasa hali yake inasikitisha.
Ndio, inaelezwa kuwa nyota huyo wa zamani aliyewahi pia kupitia Moro United kabla ya kutua Mtibwa 2007, amepatwa na tatizo la afya ya akili kwa muda mrefu kiasi cha kupelekwa katika Kituo cha Kusaidia wenye matatizo ya akili cha Mikwambe kilichopo Tuangoma, Kigamboni kwa uangalizi zaidi.
Kwa mujibu wa mtoto wa dada wa mchezaji huyo wa zamani, aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Rashid alisema mjomba’ake (yaani Idrisa) alianza kupata changamoto hiyo akiwa katika mazoezi ya timu ya AFC Leopards ya Kenya na alikuwa na ofa ya kwenda kusaini timu kubwa nje.
“Changamoto hiyo ilianza kumpata akiwa katika mazoezi na AFC Leopards ambapo wachezaji wenzake na makocha wakaanza kutokumuelewa vitu ambavyo alikuwa anavifanya kama mtu aliyechanganyikiwa.” alisema Hadija na kuongeza;
“Viongozi wa timu hiyo waliwasiliana na sisi, wakubwa zangu walisafiri hadi Kenya kwenda kumchukua, tukaanza kuhangaika naye tiba za asili ikashindikana ikabidi apelekwe Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe iliyo Dodoma ambako alikaa kwa muda mrefu hadi akawa sawa wakamruhusu kurejea nyumbani.
“Baada ya kurejea nyumbani akaa kwa muda mfupi hali ya kuchanganyikiwa ikajirudia tena tukampeleka Hospitali ya Butimba akawa anaendelea vizuri na baada ya kurejea mtaani akawa anaenda kuchukua dawa kila mwezi za kumsaidia kukaa sawa.”
Hadija alisema Idrisa kuna wakati inafikia anatembea mtupu ambapo jamii inayomzunguka inabakia kumshangaa, bila kujua kipi kimempata katika maisha yake.
“Mjomba alikuwa na mke kutoka Kenya, kutokana na hali yake akashindwa kuishi naye akaolewa Bagamoyo, hivyo alipo hana mtoto wala mke, ndio maana tunajikuta tunapata wakati mgumu hata wa kumfanyia usafi wake wa mwili,” alisema Hadija na kuongeza;
“Kwao walizaliwa watoto 10, Idrisa akiwa ni pili kutoka mwisho akiwa kijana wa kiume pekee, wenzao sita wamefariki dunia na sasa wamebakia wanne, bora wangekuwepo wazazi wao, kwani mama yake alifariki muda mrefu na baba yake alifariki Novemba mwaka jana.”
Alisema katika kituo alichopo kila mwezi wanalipia Sh500,000 ambapo tangu alipompeleka Januari wanadaiwa, kutokana na kuishiwa pesa.
“Tunaomba msaada kwa Watanzania kumsaidia Rajabu, kwani tangu alipoanza kuugua alikuwa na mashamba na magari vyote tuliviuza kwa ajili ya matibabu, lakini bado hali yake haijatengemaa,” alisema na kuongeza;
“Kama kutakuwa na mtu kaguswa kwa ajili ya kutushika mkono ili ndugu yetu asaidike basi atatutafuta kwa namba ambayo itatokea jina la 0693725803 Hadija Mwishehe.”
Timu alizocheza Mtibwa Sugar (Januari 2007- 2010), Sofapaka (2012) na AFC Leopards (2013/2014) kisha akarejea Tanzania baada ya kupata changamoto ya afya ya akili na kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars enzi za kocha Marcio Maximo.