Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Hali si shwari kwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Dk. Charles Kimei (CCM) baada ya baadhi ya wananchi wa jimbo hilo kuanza kuhoji mambo mbalimbali zikiwemo ahadi zake wakati akiomba kura mwaka 2020.
Wananchi pia wanamlalamikia mbunge huyo kuwa haonekani jimboni kutatua changamoto zao na kwenye vikao mbalimbali vya maendeleo ya wilaya, mkoa na hata baraza la madiwani amekuwa haonekani, jambo ambalo wanasema linaibua maswali mengi juu ya uwajibikaji wake.
Minong’ono kuhusu, Dk. Kimei iliibuka pia Machi,28 2025 katika kikao cha maendeleo ya Mkoa wa Kilimanjaro chini ya mkuu wake, Nurdin Babu kujadili ugawaji wa majimbo mkoani humo.
Katika kikao hicho pia RC Babu alionyesha kushangazwa na ‘utoro’ wa mbunge huyo kwenye kikao hicho muhimu ambacho muhtasari wake ulikuwa unapelekwa moja kwa moja Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa maamuzi ya mwisho.
“Ndugu wajumbe nawashukuru sana, haya ambayo tumejadiliana lazima yafike kwenye Tume Huru ya Uchaguzi, maana kuna muhtasari hapa umeandikwa, na maneno ambayo mmeyasema tutayapeleka kwenye muhtasari kama ulivyo, lakini maamuzi yatatoka kwenye Tume, ingawa yatazingatia maamuzi ya wajumbe, kwamba mwisho wajumbe walikubaliana kwamba jimbo lisigawiwe, libaki Jimbo moja la Moshi Vijijini.
“Lakini mtaalamu alichokisema na mimi pia nilitaka Dkt Kimei awepo hapa ili tujadiliane wote kwa pamoja, lakini yeye hayupo na kwenye kikao cha maendeleo ya wilaya (DCC) hayupo, kwenye baraza la madiwani pia hakuwepo, unaona hapa, sisi tunaweza kusema jimbo hilo ligawanywe, lakini huyu jamaa bado ana makali akifika kule anaweza kusema mimi sikushirikishwa,”alisema mkuu huyo wa mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe alisimama na kutoa taarifa kwa mkuu wa mkoa kuwa, si kweli kwamba Dkt Kimei hakushirikishwa kuhusu jambo hilo, isipokuwa hakutaka kushiriki.
Katika kumaliza suala hilo, RC Babu alitumia busara kwa kueleza kuwa huenda mbunge huyo hakushiriki vikao hivyo kutokana na majukumu aliyonanyo, jambo ambalo liliibua miguno na maneno ya chini chini, huku wajumbe wengi wakionyesha kutokukubaliana na hali hiyo.
Mjadala kuhusu mbunge huyo ulishika kasi hata baada ya kumalizika kwa kikao hicho huku wajumbe kadhaa wakikumbushia taarifa mbalimbali za kwenye makundi sogozi ya watsapp ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakazi wa Vunjo kwa ujumla.
Kiongozi mmoja wa CCM Vunjo ambaye hakutaka ina lake liandikwe alidokeza kuwa Dk. Kimei amekuwa akijitetea kuwa amewapa mamlaka wasaidizi wake kumwakilisha kwenye matukio yoyote pale anapokuwa hayupo.
“Nimempa Wakili, Mlaki Emmanuel na Katibu wangu madaraka ya kuniwakilisha kwenye matukio yoyote wakati ninapokuwa siko jimboni. Ninyi mnaoona wivu kuleni mate yenu wenyewe,”alinukuu ujumbe huo uliotumwa na Dk. Kimei kwa njia ya Whatsapp.
Kada huyo wa CCM alisema ujumbe huo ambao wengi wanao kwenye simu zao ni matusi na dharau ya wazi kwao kwa sababu mbunge ni mtumishi wa wanachi hivyo ni vema achunge ulimi wake.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi vijijini, Ramadhani Mahanyu alisema hawezi kuzungumzia masuala hayo ambapo alimtaka mwandishi kumtafuta mbunge mwenyewe.
“Mimi sina la kuzungumza kuhusu hilo, hivyo nakuomba umtafute mbunge mwenywe akujibu,” alisema Katibu huyo.
Alipotafuta ili kuzungumzia suala hilo Dk. Kimei hakupatikana ambapo mwandishi alimtafuta mmoja wa wasaidizi wake aliyefahamika kwa jina la Gulaton Masiga ambapo alisema suala la mbunge huyo kutokuhudhuria vikao waulizwe wanaohusika na ratiba za vikao hivyo.
“Kama ni kikao cha RCC aulizwe mkuu wa mkoa, kama ni kikao cha DCC aulizwe Afisa Tawala na kama ni vikao vya halmashauri aulizwe mkurugenzi, hao ndiyo wanazo ratiba za vikao gani mbunge alihudhuria au hakuhudhuria, mimi unaweza kuniuliza utekelezaji wa mikutano ya jimboni,” alisema Masiga na kukaa simu.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, mbunge kwa nafasi yake ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya lakini pia kwa kanuni za mabaraza ya madiwani mbunge ni mjumbe wa baraza la madiwani, mbunge pia nafasi yake ni mjumbe wa kamati ya maendeleo ya wilaya DCC, mjumbe wa kamati ya maendeleo ya mkoa (RCC).