Dar es Salaam. Wakati leo Machi 25, 2025 ikiwa ni siku ya mwisho ya uboreshaji wa daftari la mpigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya wananchi wamesema hawakupata taarifa ya uongezwaji wa siku mbili, pia shughuli zao za kila siku ndiyo zimewafanya kwenda vituoni kwa wingi hasa muda wa jioni.
Hata hivyo, wamepongeza hatua ya kuongezwa kwa muda na mashine za vitambulisho za BVR Kits zilizopunguza foleni pamoja na uhamasishaji unaofanyika kujiandikisha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Juzi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliongeza siku mbili kuanzia Machi 24 na leo 25, za uboreshaji wa daftari la mpigakura mkoani hapa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
Taarifa ya INEC ilitolewa Machi 23, 2025 na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele ikiwa ni siku moja tangu Mwananchi iripoti wingi wa watu vituoni na malalamiko ya baadhi kushindwa kuboresha taarifa zao.
Uboreshaji wa taarifa huo awali mkoani Dar es Salaam ulianza Machi 17 ambapo ulitakiwa kumalizika Jumapili Machi 23, 2025.
Hata hivyo, hadi mchana wa leo, Mwananchi imetembelea vituoni ambapo imeshuhudia watu wachache hali iliyoashiria kuwa wengi wao wameshajiandikisha.
Baada ya kuzungumza na waandikishaji na waandikishwaji wamesema kwa siku ya jana watu walimiminika wakati wa jioni baada ya kurudi kazini, ikiwa ni baada ya kupata taarifa ya uongezwaji wa muda kutoka kwa wenzao.

Walichokisema
Wakala wa kituo cha Tabata Kisiwani A, wilayani Ilala, Kato Kabwaya amesema siku mbili zilizoongezwa mwitikio wa watu umekua mkubwa hasa jioni ya jana waliporudi kutoka kazini.
“Tume imefanya jambo la muhimu kuongeza hizi siku mbili, kama si kufanya hivyo basi watu wengi wangekosa vitambulisho hasa wale wenye majukumu mengi,” amesema Kabwaya.
Ameongeza kuwa tangu jana muda wa asubuhi watu si wengi, lakini kuanzia saa 10 jioni foleni ya watu ilikuwa kubwa ingawa wanahakikisha hakuna mtu atakayeondoka pasipo kupatata kitambulisho.
Mwandikishaji Mohamed Hamidu kutoka kituo cha Dar es Salaam International School chenye kituo A na B kilichopo Kata ya Sinza wilayani Ubungo amesema watu wengi wamekuja hasa jana Jumatatu.
“Kituo hiki kina mashine jumla nne watu kama unavyoona wanaenda wanapungua kwa kuwa wanaambizana wanakuja. Wengine wanasema hawakupata taarifa ila hadi sasa tamko la tume lina tija,” amesema Hamidu.
Omary Shabani (57) mkazi wa Mtaa wa Mabibo amesema kama siyo kuongezwa muda basi yeye alikuwa ameshakosa kitambulisho, huku akisema sababu kubwa ya yeye kutojiandikisha amedai kuwa ni majukumu.

“Sijawahi kumiliki kitambulisho cha kupiga kura hivyo leo kama nitapata itakuwa mara yangu ya kwanza kumiliki,” amesema Shabani.
Katika kituo cha Shule ya Msingi Ubungo Kisiwani chenye mashine nane kilichopo Mtaa wa Kibangu, Kata ya Makuburi kimesema kimeandikisha vijana wengi zaidi.
Mmoja ya msimamizi ambaye hakutaka jina lake litwaje kutoka Mabibo A, amesema Watanzania wengi wanapenda kusukumwa kwani hawapendi kufanya majukumu yao mapema na kwa wakati.
“Watanzania wanapenda kusukumwa maana ile siku ya mwisho ya Machi 23 watu walikuwa wengi hadi tukawaambia njooni kesho kwani siku zimeongezwa baada ya kuongezwa siku hatuwaoni,” amesema msimamizi.
Mkazi wa Mtaa wa Muongozo, Kata ya Makuburi Wilaya ya Ubungo, Iddi Ginaley (27) amesema kuongezwa kwa siku mbili ni bahati kwake amepata kitambulisho.
“Nashukuru siku za nyongeza ambazo zimetolewa na Tume zimenisaidia kwa kweli kwani nilibahatika kupata kitambulisho mapema,” amesema Ginaley.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Madenge Buguruni Rehema Ally, amesema hapo mwanzo foleni ilikuwa kubwa, lakini baada ya kuongezwa kwa mashine katika kituo hiko sasa foleni imepungua kabisa.
“Tulikuwa tunatumia mashine moja ndiyo sababu kubwa ya foleni, lakini juzi jioni tumeongezwa mashine moja sasa zipo mbili ndiyo maana unaona watu hakuna kabisa,” amesema Rehema.
Sambamba na hayo amesema pia baadhi ya watu hawajapata taarifa ya kuongezwa kwa siku mbili ndiyo maana hakuna idadi kubwa ya watu kwa baadhi ya vituo.
Awali, tume ilisema kutokana na mwitiko mkubwa ilichukua hatua za kuongeza mashine hizo pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii imewezesha shughuli hiyo kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote.
Hatua hiyo imewezesha kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano kwenye baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, wito wa tume kuongeza muda uliambatana na onyo kwa wananchi kutokujiandikisha zaidi ya mara moja kwani ni kosa na mtu akibainika anaweza kufungwa, kutozwa faini au vyote viwili kutupwa jela na kutozwa faini.