Hali ilivyo nyumbani kwa Mafuru

Dar es Salaam. Maandalizi ya kupokea mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru yanaendelea nyumbani kwake, huku waombolezaji kadhaa wakijitokeza kuipa faraja familia leo Jumatatu, Novemba 11, 2024.

Mwananchi imefika nyumbani kwa Mafuru, Bunju A jijini Dar es Salaam na kukuta maandalizi mbalimbali yakiendelea, ikiwa ni pamoja na kuandaa eneo la watu kusaini kitabu cha maombolezo, na kuwekwa mahema pamoja na mapambo.

Walinzi wa moja ya kampuni ya ulinzi nchini walikuwa getini kutoa maelekezo na kuwapokea waombolezaji waliokuwa wakifika nyumbani hapo.

Hali ya ukimya imeendelea kutawala nyumbani kwa marehemu huku nyimbo za maombolezo zikipigwa.

Mafuru alifariki dunia Novemba 9, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo nchini India, mwili wake utazikwa Ijumaa, Novemba 15 katika makaburi ya Kondo yaliyopo Tegeta, jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini kesho Jumanne.

Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwa nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, marehemu Lawrence Mafuru, eneo la Bunju A, jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Novemba 11, 2024. Picha na Sunday George

Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi maarufu hapa nchini akihudumu katika sekta binafsi na sekta ya umma, mwili wake utawasili nchini kesho saa 7:45 mchana katika uwanja vya ndege vya kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ukitokea New Delhi, India na utakwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Lugalo.

Jumatano itakua ni maombolezo nyumbani kwa marehemu Bunju A na Alhamisi Novemba 14, mwili wa Mafuru utaagwa katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana, kisha utapelekwa nyumbani kwake utakapolala kabla ya maziko kufanyika Ijumaa.

Ratiba ya mazishi itaanza saa 2:00 asubuhi kwa chai kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu na saa 4:30 hadi saa 5:30 asubuhi msafara wa marehemu na waombolezaji kuelekea Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Magomeni ambapo itafanyika ibada ya faraja kuanzia saa 6:00 hadi saa 8:00 mchana na msafara utaelekea makaburi ya kwa Kondo, Tegeta tayari kwa  maziko kuanzia saa 9:00 alasiri.

Mafuru amefariki dunia akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, ambaye amehudumu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu.

Katika eneo ambalo alikuwa anahudumu, miongoni mwa kazi zinazofanywa na ofisi ya Tume ya Mipango ni kuandaa dira ya maendeleo ya Taifa ya muda mfupi na muda mrefu, Mafuru amefariki wakati mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ukiendelea.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema, Mafuru ni miongoni wa Watanzania wabobevu wenye maarifa na amefariki dunia katikati ya shughuli ya kuandaa dira hiyo ya Taifa.

Amesema uwezo wake ndani ya Serikali na sekta binafsi ulimfanya kuheshimika na kufanya kazi zake kwa weledi.