Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.

Msuya alifariki dunia Jumatano, Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo, mwili unaagwa leo Jumapili, Mei 11, 2025 kitaifa, utazikwa Jumanne ya Mei 13,2025 kijijini kwao Usangi Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Miongoni mwa waliofika kwenye viwanja hivyo ni Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza waombolezaji kuaga mwili wa kiongozi huyo mstaafu, aliyefariki akiwa na miaka 94.

Baada ya Rais kuwasili, jeneza lenye mwili wa Msuya limeletwa viwanjani hapo waombolezaji wakaimba wimbo wa Taifa na kisha ibada kuendelea.
Hali ilivyo
Hali ni ya utulivu katika barabara ulipo ukumbi wa Karimjee, huku baadhi ya maeneo yakiwa yamezungushiwa utepe mwekundu kutoruhusu magari yasiyohusika na msiba kupita.

Nje ya uwanja huo, kumetungushwa machuma ya njia ya watembea kwa miguu, huku kila muombolezaji akitakiwa kutumia sanitaiza mlangoni kabla ya kuingia na kukaguliwa kwenye skana.

Wafanyabiashara ndogondogo nao hawajabaki nyuma wamejitokeza eneo hilo wakiuza beji zenye picha ya Msuya na wengine wakiuza leo kwa kila moja Sh1,000.
Endelea kufuatilia Mwananchi