‘Haki za watoto wenye uhitaji zitambuliwe’

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inaendelea kufanya kazi na wadau kuhakikisha haki za watoto wenye uhitaji maalumu zinatambuliwa na kuzingatiwa katika sera na mipango ya maendeleo.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul ametoa kauli hiyo jana Jumapili Machi 23, 2025 wakati wa akizungumza katika hafla ya kufuturisha iliyoendana na maadhimisho ya Siku ya Watoto wenye Sura Mfanano, iliyoandaliwa na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Unguja.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inaendelea kuimarisha huduma za afya, elimu na ustawi wa jamii kwa watoto na watu wenye uhitaji maalumu,” amesema.

Amesema pamoja na kuadhimisha siku hiyo pia ni vyema kuenzi utu, haki na fursa kwa kila mtoto na mtu mwenye ulemavu kwa kuwa, kila mmoja ana haki ya kuishi kwa heshima na kupata elimu, huduma na fursa sawa na wengine.

“Watu wenye sura mfanano ni sehemu ya jamii na wanapaswa kujivunia, kuthaminiwa na kuungwa mkono kwa kila hatua wanazozichukua,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation, Asma Ali Hassan Mwinyi amesema wataendelea kuwaunga mkono watoto hao na kuthamini utu wao.

Wakati huohuo, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kushirikiana na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation imewapatia msaada wa vitu mbalimbali yatima, wajane, wazee na  watu wenye uhitaji maalumu Mkoa wa Kusini Unguja.

 Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation, Asma Ali Hassan Mwinyi  amesema benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa msaada kwa watu na makundi mbalimbali ili kuona na wao wanakuwa kama watu wengine.

“Tutaendelea kuwahamasisha wadau wengine mbalimbali kuona wananchi wanaohitaji wanapata misaada kama hiyo katika shehia nyingine,” amesema.

Baadhi ya wananchi waliopatiwa msaada huo akiwamo Ali Mohamed Ali alishukuru na kuahidi kutumia kama ilivyokusudiwa na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza kwa kwenda kuwafariji na ukizingatia huu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mwalimu wa Madrasa ya Maftaha, Amina Nahodha Makame amesema amewaomba kuendelea kuwa na moyo wa imani na wasichoke kuwasaidia katika kuwapatia misaada.

Sheha wa Shehia ya Muyuni C, Hassan Amour Ali amesema kuyapatia msaada makundi hayo ni faraja kwa kuwa shehia yake kuna uhitaji mkubwa.

Hivyo, aliziomba taasisi nyingine kuiga mfano wa taasisi ya PBZ na Asma Mwinyi Foundation, na kuishukuru kwa msaada huo.

Jumla ya wananchi 60 wa shehia ya Muyuni C, wamepatiwa msaada ikiwamo sukari, unga wa ngano, mafuta ya kula na mchele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *